AU yasikitishwa na miripuko ya E/Guinea, walioaga dunia wakaribia 100
(last modified Tue, 09 Mar 2021 03:28:25 GMT )
Mar 09, 2021 03:28 UTC
  • AU yasikitishwa na miripuko ya E/Guinea, walioaga dunia wakaribia 100

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika miripuko kadhaa iliyotokea kwenye kambi moja ya kijeshi huko nchini Equatorial Guinea imeongezeka na kufikia watu 98.

Hayo yamethibitishwa na Wizara ya Afya ya nchi hiyo ambayo imeongeza kuwa, watu zaidi ya 600 wamejeruhiwa pia katika miripuko hiyo iliyotokea juzi Jumapili katika kambi ya jeshi ya Nkoantoma iliyoko katika mji wa Pwani wa Bata.

Wizara hiyo imesema imeandaa timu ya madaktari, wauguzi na hata wanasaikolojia wa kuwapa ushauri nasaha waathirika wa mkasa huo ikisisitiza kuwa, miripuko hiyo mbali na kuwasababishia majeruhi makovu ya miili, lakini pia imewaathiri kiakili.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika sanjari na kuelezea kusikitishwa mno na miripuko hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia jana, lakini pia ametoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa miripuko hiyo.

Mamia ya watu wamejeruhiwa katika miripuko hiyo ya baruti E/Guinea

Katika ujumbe wa Twitter jana Jumatatu, Moussa Faki Mahamat amesema: Tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa familia za wahanga na wapendwa wao, taifa na serikali ya Equatorial Guinea kufuatia miripuko mibaya ya Bata.

Kuna wasi wasi wa kuongezeka idadi ya wahanga wa mkasa huo ulioikumba nchi hiyo ndogo ya Kiafrika yenye jamii ya watu milioni 1.4, kwani timu za maafisa usalama na asasi za kiraia zinaendelea kupekua vifusi vya majengo yaliyokumbwa na miripuko hiyo ya baruti.