Uzalishaji mafuta Nigeria washuka kutokana machafuko Niger Delta
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6805-uzalishaji_mafuta_nigeria_washuka_kutokana_machafuko_niger_delta
Uzalishaji mafuta ghafi ya petroli Nigeria unatarajiwa kufika kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka 22 iliyopita kutokana na hujuma za waasi katika eneo lenye utajiri wa mafuta la Niger Delta.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2016 10:32 UTC
  • Uzalishaji mafuta Nigeria washuka kutokana machafuko  Niger Delta

Uzalishaji mafuta ghafi ya petroli Nigeria unatarajiwa kufika kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka 22 iliyopita kutokana na hujuma za waasi katika eneo lenye utajiri wa mafuta la Niger Delta.

Duru zinaarifu kuwa mwezi huu wa Mei Nigeria inatarajiwa kuzalisha mapipa milioni 1.69 kwa siku na kwamba kwa kuzingatia uvurugaji unaofanywa, uzalishaji huo utafika mapipa milioni 1.46 kama ilivyokuwa mwaka 1994.

Mashirika yanayozalisha mafuta kusini mwa Nigeria katika eneo la Niger Delta yametakiwa kuondoa wafanyakazi wao katika vituo kadhaa vya mafuta kutokana na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa sekta hiyo. Wiki iliyopita kundi la waasi wajulikanao kama Walipizaji Kisasi wa Niger Delta walishambulia kituo cha mafuta cha shirika la Kimarekani la Chvron baada ya kudai kuhusika na hujuma dhidi ya bomba la mafuta la shirika la Uingereza na Uholanzi la Shell.

Chika Oneugbu, mwenyekiti wa Jumuiya za Wafanyakazi katika jimbo la Rivers eneo la Niger Delta amesema mashirika mengi yameanza kuondoa wafanyakazi wao katika eneo hilo na jambo hilo litapelekea kupungua kiwango cha uzalishaji mafuta.

Eneo la Niger Delta liko kusini mwa Nigeria na lina majimbo tisa ambayo yanaongoza kwa hifadhi ya mafuta nchini humo.

Ni miongo minne sasa tokea Nigeria igundue mafuta na ianze kuyachimba na kuyauza katika masoko ya kimataifa. Lakini Wanigeria bado hawajafaidika ipasavyo na utajiri huo wa kitaifa wa nchi yao.