Makumi wapoteza maisha kutokana na athari za mvua Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6850-makumi_wapoteza_maisha_kutokana_na_athari_za_mvua_ethiopia
Kwa akali watu 50 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 11, 2016 07:05 UTC
  • Makumi wapoteza maisha kutokana na athari za mvua Ethiopia

Kwa akali watu 50 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Ethiopia.

Alemayehu Mamo, Mkuu wa Jeshi la Polisi katika eneo la Wolayita, kusini mwa Ethiopia amesema watu zaidi ya 40 wamefariki dunia kutokana na maporomoko ya ardhi katika kanda hiyo.

Duru za habari zinaarifu kuwa, karibu watu 10 wengine wameaga dunia kutokana na mafuriko katika eneo la Bale, kusini mashariki mwa nchi. Aidha mifugo zaidi ya 1,000 wamesombwa na mafuriko katika eneo hilo.

Habari zaidi zinasema kuwa, makumi ya maelfu ya watu wameachwa bila makazi kutokana na taathira hasi za mvua hizo katika maeneo mbali mbali ya nchi, mbali na kuathiriwa kwa miundomsingi kama vile barabara na kuporomoka kwa madaraja.

Haya yanajiri siku chache baada ya watu zaidi ya 30 kupoteza maisha na mamia ya wengine kuachwa bila makazi kufuatia maporomoko ya ardhi na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini Rwanda.

Makumi ya watu wamepoteza maisha na maelfu ya wengine wamebaki bila makazi kutokana na mvua hizo zinazoendelea kunyesha katika nchi za kanda ya Afrika Mashariki na Kati.