7 wauawa baada ya waasi kushambulia kambi za jeshi CAR
Watu wasiopungua saba wameuawa katika msururu wa mashambulio ya genge moja la waasi mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Msemaji wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo (MINUSCA), Abdoulaziz Fall amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, kundi la waasi la Unity for Peace in Central Africa (UPC) hapo jana lilitekeleza wimbi la hujuma dhidi ya vituo vya upekuzi na kambi za kijeshi katika mji wa Alindao, mashariki mwa nchi ambapo watu saba wameuawa.
Ameongeza kuwa, askari wapatao 60 wa MINUSCA wametumwa katika mji huo kwenda kupiga jeki operesheni ya kuwafurusha waasi hao, na kwamba kufikia sasa wamefanikiwa kuwarudisha nyuma wapiganaji hao umbali wa kilomita tatu.
Katika hatua nyingine, serikali ya CAR hapo jana ilikadhibisha vikali madai ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwamba wanajeshi wa serikali ya nchi hiyo pamoja na wale wa Russia wamekanyaga haki za binadamu. Taarifa ya serikali ya nchi hiyo imesema madai hayo yametolewa kwa lengo la kulichafulia jina taifa hilo na wala hayana msingi wowote.
Hivi karibuni pia, Ikulu ya Russia (Kremlin) ilikanusha madai kwamba wakufunzi wa kijeshi wa nchi hiyo waliopo Jamhuri ya Afrika ya Kati wamehusika katika mauaji ya raia na kupora mali za watu majumbani.
Marekani, Ufaransa na Uingereza zimewatuhumu wakufunzi wa kijeshi wa Russia kwa kukiuka haki za binadamu na kuwazuia wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yao huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Jamhuri ya Afrika ya Kati yenye utajiri wa madini imekuwa katika mgogoro na mapigano ya kidini na kikabila tokea mwaka 2013.