Wanamgambo wa ash Shabab wa Somalia kusamehewa lakini...
Rais Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia amesema kuwa, yuko tayari kutoa msamaha kwa wanamgambo wa Somalia lakini kwa sharti waweke chini silaha na kuacha mashambulizi.
Shirika la habari la Xinhua limemnukuu Rais Mahamud akisema hayo na kuongeza kuwa, serikali ya Somalia haitawafuatilia kisheria wanamgambo wa ash Shabab wanaoweka chini silaha zao na kuacha mashambulizi.
Ameongeza kuwa, vijana wote waliojiunga na kundi hilo watasamehewa iwapo watatimiza masharti ya msamaha uliotolewa na serikali.
Mwaka jana pia serikali ya Somalia ilitoa msamaha kama huo kwa wanamgambo wa ash Shabab wanaojitoa kwenye kundi hilo na kukabidhi silaha zao.
Kabla ya hapo kamanda mmoja wa ngazi ya juu wa jeshi la Somalia, aliwahi kusema kuwa, mashambulizi makali dhidi ya kundi la ash-Shabab, yamekuwa na mafanikio makubwa. Dahir Muhammad, alisema siku ya Jumamosi kuwa, kundi la ash Shabab limekumbwa na wasi wasi mkubwa kutokana na mafanikio ya jeshi la serikali hususan katika eneo la Shabelle la kusini mwa Somalia ambalo ni ngome ya wanamgambo hao.
Eneo la Shabelle limeshuhudia mashambulizi makali ya jeshi la serikali ya Somalia kwa kushirikiana na askari wa Umoja wa Afrika, AMISOM, katika siku za hivi karibuni.