Wafuasi wa Zuma waandamana Afrika Kusini kumtetea kiongozi wao aliyefungwa jela
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i72220-wafuasi_wa_zuma_waandamana_afrika_kusini_kumtetea_kiongozi_wao_aliyefungwa_jela
Wafuasi wa rais wa zamani wa Afrika Kusini walifanya maandamano jana Jumamosi katika mkoa wa KwaZulu Natal wakipinga kufungwa jela mwanasiasa huyo anayetuhumiwa kuhusika na ufisadi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2021 00:13 UTC
  • Wafuasi wa Zuma waandamana Afrika Kusini kumtetea kiongozi wao aliyefungwa jela

Wafuasi wa rais wa zamani wa Afrika Kusini walifanya maandamano jana Jumamosi katika mkoa wa KwaZulu Natal wakipinga kufungwa jela mwanasiasa huyo anayetuhumiwa kuhusika na ufisadi.

Waandamanaji hao walichoma moto magari yakiwemo malori kadhaa wakitaka Jacob Zuma aachiwe huru. 

Ripoti zinasema kuwa, tangu Alkhamisi iliyopita wafuasi wa Zuma walifunga barabara nyingi za kuingia katika mkoa huo wa KwaZulu Natal wakipinga kufungwa jela rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini.

Wiki iliyopita Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini iliagiza Zuma afungwe jela kwa kukataa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ufisadi uliofanyika katika kipindi chake cha uongozi kutoka 2009 hadi 2018. 

Zuma, 79, anakanusha kuhusika na ufisadi na amesema kuwa ni mhanga wa njama za kisiasa.

Rais mstaafu wa Afrika kusini Jacob Zuma, alijikabidhi kwa polisi siku kadhaa zilizopita na kupelekwa katika gereza lililo karibu na nyumbani kwake katika jimbo la KwaZulu Natal.

Jacob Zuma

Hukumu dhidi ya Zuma ambayo ni ya kwanza dhidi ya rais wa zamani wa nchi huko Afrika Kusini, ilizua mtafaruku wa kisheria na kufuatiwa na maandamano makubwa ya wafuasi na watetezi wa mwanasiasa huyo.

Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini alilazimika kujiuzulu mwezi Februari mwaka 2018 kutokana na mashinikizo ya chama tawala cha ANC kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi na utumiaji mbaya wa madaraka yake.