Waliouawa katika ghasia za Afrika Kusini wapindukia 330
Serikali ya Afrika Kusini imetangaza kuwa, idadi ya watu waliouawa katika ghasia zinazoendelea nchini humo imepindukia 300.
Hayo yametangazwa na Khumbudzo Ntshavheni, Waziri wa Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini katika kikao na waandishi wa habari jana Alkhamisi na kufafanua kuwa, baada ya siku 14 za ghasia za kulalamikia kufungwa Jacob Zuma rais mstaafu wa nchi hiyo, idadi ya watu waliouawa katika fujo hizo kufikia leo (jana Alkhamisi) imefikia 337.
Siku moja kabla, yaani siku ya Jumatano, serikali ya Afrika Kusini ilikuwa imetangaza kuwa, idadi ya waliouawa kwenye ghasia na makabaliano hayo baina ya waandamanaji na maafisa usalama wakiwemo wanajeshi ni 276.
Kadhalika mamia ya watu wametiwa mbaroni wakihusishwa na ghasia hizo zilizoandamana na uporaji na uharibifu wa mali za umma hususan katika mikoa mikubwa ya Gauteng na KwaZulu-Natal.

Hii ni licha ya Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kusema hivi karibuni kuwa, utulivu umerejea katika aghalabu ya miji ya nchi hiyo iliyokumbwa na ghasia na machafuko kulalamikia kufungwa Zuma rais mstaafu wa nchi hiyo.
Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini iliagiza Rais mstaafu wa nchi hiyo, Jacob Zuma afungwe jela kwa kukataa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ufisadi uliofanyika wakati wa uongozi wake kuanzia mwaka 2009 hadi 2018.