Serikali ya Nigeria yawaonya wafanya mgomo
Serikali ya Nigeria imetoa onyo kali kwa vyama vya wafanyakazi na vya ushirika vilivyosema kuwa vitaendelea na mgomo wa nchi nzima kwa ajili ya kupigania haki zao.
Shirika la habari la Ufaransa limeinukuu taarifa iliyotolewa leo na serikali ya Nigeria ikisema kuwa, watu wanaoendelea na mgomo wajiandae kwa majibu makali kutoka kwa serikali.
Vyombo vya mahakama vya Nigeria pia, jana Jumanne vilitangaza kuwa, mgomo ulioitishwa na vyama vya wafanyakazi na vya ushirika, ni kinyume cha sheria.
Vyama hivyo vimeitisha mgomo huo kulalamikia kupanda kwa asilimia 67 ya bei ya mafuta nchini humo.
Kabla ya hapo, baadhi ya vyama vya wafanyakazi vilikuwa vimewataka wananchi wa Nigeria kuendelea na mgomo wao, kama mazungumzo baina yao na serikali yatashindwa.
Ofisi za serikali, viwanja vya ndege, bandari, mabenki, maduka ya rejareja pamoja na masoko, ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki kwenye mgomo huo.
Nigeria inahesabiwa kuwa na uchumi mzuri zaidi barani Afrika, lakini kuporomoka bei ya mafuta katika soko la dunia kumetoa pigo kubwa kwa uchumi wa nchi hiyo.