Oct 19, 2021 13:31 UTC
  • Jeshi la Nigeria laangamiza makumi ya wanamgambo kaskazini mwa nchi

Wanamgambo 24 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram na genge hasimu Daesh huko magharibi mwa Afrika maarufu kwa jina la ISWAP wameuawa katika operesheni mbili za wanajeshi wa Nigeria, kaskazini mashariki mwa nchi.

Meja Jenerali Christopher Musa, kamanda wa kikosi kazi cha kupambana na magenge ya kigaidi nchini Nigeria amesema leo Jumanne kuwa, wanachama 16 wa Boko Haram wameangamizwa katika operesheni ya kwanza ya wanajeshi wa Nigeria karibu na mji wa Maiduguri, makao makuu ya mkoa wa Borno. 

Naye Brigedia Jenerali Onyema Nwachukwu, msemaji wa jeshi la Nigeria amesema askari wa nchi hiyo wakishirikiana na wenzao wa Cameroon jana Jumatatu walifanikiwa kuangamiza wanachama wanne wa ISWAP walipojaribu kuvamia kambi ya kikosi hicho cha pamoja mkoani Borno.

Amesema wanachama wengine wanne wa genge hilo waliangamia baada ya gari lao lililokuwa limesheni mada za mlipuko, bunduki na zana zingine za kijeshi kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika mkoa huo. 

Baadhi ya wanachama wa ISWAP

Wiki iliyopita, jeshi la Nigeria pasi na kutoa maelezi ya kina, lilitangaza habari ya kuangamizwa kiongozi wa genge la kigaidi la ISWAP, Abu Musab al Barnawi, mkuu wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) huko kaskazini mwa nchi.

Mwaka 2016 genge la Daesh (ISIS) lilijiengua kutoka kwenye genge la Boko Haram na kuanzisha genge jipya la kigaidi  lililolipachika jina la ISWAP.

Tags