Kenya yajibu mapigo, yasimamisha safari za ndege kutoka Imarati
Kenya imesimamisha safari zote za ndege za abiria kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu, kujibu hatua ya Imarati ya kuzuia kwa muda usiojulikana ndege zote za kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki kutua nchini humo, kwa madai ya vyeti bandia vya Corona.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Safari za Anga ya Kenya (KCAA), Gilbert Kibe, amesema agizo hilo limeanza kutekelezwa saa sita usiku wa kuamkia leo Jumanne.
Kibe amesema agizo hilo la kusimamisha safari zote za ndege za abiria kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu litadumu kwa muda wa siku saba.
Hata hivyo amesisitiza kuwa agizo hilo halijaathiri safari za ndege za mizigo zinazotoka Imarati kwenda nchini humo.
Haya yanajiri siku chache baada ya Imarati kusimamisha safari zote za ndege kutoka Kenya, baada ya kugundua kuwa, baadhi ya wasafiri waliowasili katika nchi hiyo ya Kiarabu ya Asia Magharibi hivi karibuni, walikuwa na ugonjwa wa Covid-19, licha ya vyeti vyao vya vipimo vya PCR kuonesha kuwa hawajaambukizwa.
Wizara ya Afya ya Kenya tayari imeanzisha uchunguzi wa kuwabaini na kuwafikisha mbele ya sheria maafisa usalama waliohusika kwenye sakata hilo la vyeti ghushi vya vipimo vya maradhi ya ugonjwa wa Covid-19.