Wapinzani Brazaville wataka mazungumzo ya kisiasa
Mratibu wa Muungano Mkuu wa upinzani nchini Kongo Brazaville amesema kuwa muungano huo upo tayari kufanya mazungumzo ili kuhitimisha mgogoro wa kisiasa nchini humo.
Charles Zacharie Bowao ameongeza kuwa iwapo pande zote husika zitakuwa na wasiwasi kuhusu maslahi ya pamoja ya taifa, basi muungano mkuu wa upinzani nchini Congo Brazaville nao utatafuta njia za kupatikana suluhu ili kumaliza mgogoro wa hivi sasa nchini humo.
Kiongozi huyo wa kambi ya upinzani amesisitiza pia kuwa, muungano wao hauna lengo la kuitumbikiza nchi hiyo vitani na kusababisha umwagaji damu nchini. Mgogoro wa kisiasa ulishtadi huko Congo Brazaville baada ya kutangazwa mshindi Denis Sassou Ngueso katika uchaguzi wa mwezi Machi 20 mwaka huu. Kabla ya kufanyika uchaguzi huo wa rais, wapinzani wa serikali ya Brazaville walisema hatua ya kiongozi huyo ya kugombea kiti hicho kwa mara ya tatu mfululizo inakiuka katiba ya Jamhuri ya Congo.