Wanamgambo washambulia bomba la mafuta, Niger Delta Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8005-wanamgambo_washambulia_bomba_la_mafuta_niger_delta_nigeria
Wanamgambo wameshamulia bomba muhimu la mafuta katika eneo la Niger Delta nchini Nigeria huku kundi la wanamgambo linalojiita Walipiza Kisasi wa Niger Delta likitangaza kuhusika na hujuma hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 28, 2016 23:23 UTC
  • Wanamgambo washambulia bomba la mafuta, Niger Delta Nigeria

Wanamgambo wameshamulia bomba muhimu la mafuta katika eneo la Niger Delta nchini Nigeria huku kundi la wanamgambo linalojiita Walipiza Kisasi wa Niger Delta likitangaza kuhusika na hujuma hiyo.

Wakaazi wa jimbo la Bayelsa kulikotokea mashambulizi hayo, wanasema kwamba, walisikia miripuko kadhaa wakati wa usiku katika eneo la bomba hilo ambalo husafirisha mafuta ghafi ya Bonny Light.

Shirika la mafuta la Uingereza na Uholanzi la Royal Dutch Shell, ambalo husafirsha mafuta hayo ya Bonny Light, halijatoa taarifa yoyote kuhusu tukio hilo.

Kundi la wanamgambo wanaojiita Walipiza Kisasi wa Niger Delta pamoja na makundi mengine ambayo yanasema yanaendesha mapambano kudai fungu kubwa zaidi la faida ya mafuta, kuhitimisha uchafuzi wa mazingira na kutaka kujitawala eneo la Niger Delta, yameshadidisha mashambulio yao katika miezi ya karibuni na kusababisha kupungua uzalishaji wa mafuta na kufikia kiwango cha chini zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita na kuifanya hali ya uchumi wa Nigeria iwe mbaya zaidi.

Wakaazi wa eneo la Delta, ambao baadhi yao wanayaunga mkono makundi ya wanamgambo, wamekuwa kwa muda mrefu wakilalamikia hali ya umasikini ya eneo lao hilo ambalo linazalisha mafuta yanayodhamini asilimia 70 ya pato lote la taifa la Nigeria.