Zanzibar yazindua teknolojia mpya ya kupima corona kwa simu
Serikali ya Zanzibar jana Jumatano ilizindua rasmi teknolojia mpya inayoweza kutambua uwezekano wa maambukizi ya Covid-19 kwa muda mfupi kwa kutumia simu (EDE).
Teknolojia hiyo, tofauti na nyengine, haihitaji msafiri kuchukuliwa sampuli ya vipimo kupitia mdomoni au puani, na vilevile anaweza kupimwa akiwa umbali wa mita moja na majibu yake yanatolewa hapo kwa hapo.
Hii ni mara ya kwanza kwa teknolojia hii kutumika barani Afrika, na Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ndio unaandika historia ya kuwa uwanja wa kwanza wa kimataifa nchini Tanzania kuwa na teknolojia hiyo.
Inaaminika kwamba, matumizi ya teknolojia hiyo, yanaweza kuleta afueni kubwa kwa wasafiri ambao kwa sasa wataweza kuendelea na safari zao kwa haraka zaidi bila usumbufu na kupoteza muda.
Wakati huo hio Serikali ya Zanzibar imeeleza kuwa hivi sasa hakuna mgonjwa hata mmoja wa ugonjwa wa uviko-19 lakini haiwezi kusema ugonjwa huo umeisha visiwani humo kwa kuwa huzuka na kupotea.
Hayo yalielezwa na Rais Dk Hussein Mwinyi jana Februari 16, 2022 wakati wa mahojiano yake na waandishi wa habari, Ikulu Zanzibar.
Dk Hussein Ali Mwinyi alisema: "Kwa Zanzibar sasa maambukizi yapo chini, kipimo cha ugonjwa ni kuangalia wagonjwa waliopo hospitali, kwa sasa hakuna hata mmoja aliyelazwa."
Zanzibar, kama maeneo mengine ya Tanzania, ilikumbwa na wingi la maambukizi ya Covid-19 tangu kuanza kuibuka kwa kirusi hicho.
Mwaka jana, wakati kama huu, Zanzibar ilimpoteza makamu wake wa rais wa kwanza Maalim Seif Sharif Hamad ambae aliaga dunia kutokana na maambukizi ya Covid-19.