Mar 09, 2022 10:22 UTC
  • Watu 16 wauawa katika mapigano ya kikabila Darfur, Sudan

Watu wasiopungua 16 wameuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa katika mapigano ya kikabila katika mkoa wa Darfur Magharibi nchini Sudan.

Taarifa ya Kamati ya Madaktari Darfur Magharibi imesema watu zaidi ya 16 wameuawa huku wengine 16 wakijeruhiwa katika wimbi hilo jipya la mapigano ya kikabila katika eneo hilo baina ya Machi 5 na 7.

Adam Rigal, Msemaji wa Kamati Kuu ya Wakimbizi wa Darfur amewatuhumu waasi wenye mfungamano na vyombo vya usalama vya serikali katika eneo hilo kuhusika na mauaji hayo.

Hitilafu za kugombania ardhi baina ya makabila ya Waarabu na wasio Waarabu katika eneo lenye milima mingi ya Jebel Moon mkoa wa Darfur Magharibi zimesababisha mapigano ya umwagaji damu na mauaji ya mamia ya watu tokea Novemba mwaka jana hadi sasa.

Machafuko Darfur

Eneo la Darfur mwaka 2003 lilikumbwa na mapigano ya umwagaji damu kati ya serikali ya wakati huo ya Sudan chini ya uongozi wa Rais aliyeenguliwa mdarakani, Omar Hassan al-Bashir, na wapinzani wa serikali.

Malaki ya watu waliuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi katika mashambulizi hayo, na tokea wakati huo, eneo hilo limekuwa uwanja wa mapigano na umwagaji damu.

Tags