Mazungumzo ya amani ya CAR yamalizika pasina na matunda yoyote
(last modified Tue, 29 Mar 2022 01:30:45 GMT )
Mar 29, 2022 01:30 UTC
  • Mazungumzo ya amani ya CAR yamalizika pasina na matunda yoyote

Mazungumzo ya amani katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati iliyoathiriwa na vita vya ndani vinavyoendelea tangu mwaka 2013 yamemalizika pasina na kuchukuliwa na maamuzi muhimu.

Mazungumzo hayo ambayo yalianza juzi Jumapili yalimalizika jana Jumatatu na hakuna kundi la waasi lililoalikwa kushiriki mazungumzo hayo huku vyama vya upinzani pia vikiyasusia. Mwishoni mwa mwaka 2020, Rais Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliahidi kufanya mazungumzo ili kurejesha amani nchini humo baada ya kuchaguliwa  tena kuwa rais katika uchaguzi ulioibua utata. 

Rais Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Tarehe 15 mwezi huu wa Machi Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati alitangaza kuwa mazungumzo ya amani kati ya serikali ya nchi hiyo, mrengo wa upinzani na jumuiya za kiraia yataanza tarehe 21 mwezi huu wa Machi. Pamoja na hayo  ajenda ya mazungumzo imesalia mezani bila ya kupigwa hatua yoyote ya msingi. 

Mazungumzo ya amani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo yalifanyika katika Bunge la Taifa la nchi hiyo katika mji mkuu Bangui yaligubigwa na mivutano pale pendelezo la kuifanyia mabadiliko katiba ili kumruhusu rais kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu lilipowalishwa katika majadiliano ya awali. Hata hivyo pendekezo hilo baadaye liliondolewa. 

Mwenyekiti wa mazungumzo ya amani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Richard Filkota, alisema wakati wa kufunga kikao hicho kwamba, jumla ya mapendekezo 600 yamewasilishwa katika kikao hicho. Moja ya mapendekezo hayo ni kutaka kuhitimishwa vikwazo vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa mwaka 2013 baada ya muungano wa makundi yanayobeba silaha kuipindua serikali ya Rais Francois Bozize na kuitumbukiza nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.