Rais Kais Saied wa Tunisia avunja Bunge, asema kuna jaribio la mapinduzi
(last modified Thu, 31 Mar 2022 03:12:08 GMT )
Mar 31, 2022 03:12 UTC
  • Kais Saied
    Kais Saied

Rais wa Tunisia, Kais Saied jana Jumatano alitangaza kuvunja Bunge muda mfupi baada ya bunge hilo kupitisha sheria ya kufuta hatua za dharura zilizotangazwa na kiongozi huyo majira ya joto mwaka jana.

Saied alitangaza kuvunjwa kwa Bunge wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama la Kitaifa, na akasema kwamba amechukua uamuzi huo kwa kuzingatia Sura ya 72 ya Katiba "ili kulinda Serikali na taasisi zake." 

Ameongeza kuwa Tunisia imo katika hali ya kipekee na katika "jaribio la mapinduzi," na kusema kuwa wabunge waliofanya kikao jana "wanajua kuwa hawana uhalali, na wanachofanya sasa na watakachofanya baadaye, hakina thamani ya kisheria." 

Rais wa Tunisia ameonya kwamba njia yoyote ya kufanya vurugu itakabiliwa na sheria na nguvu ya vikosi vya jeshi, na kusema kwamba "serikali sio mchezo kwa wale wanaojaribu kuipindua."

Akijibu hatua hiyo ya Kais Saied, mjumbe wa Ofisi ya Mtendaji wa harakati ya Ennahda, Ahmed Qaaloul, amesema harakati hiyo itaendeleza upinzani wa amani na wa kiraia na kutoa wito wa mazungumzo.

Watunisia wanapinga maamuzi ya Kais Saied

Katika kikao cha mashauriano kilichofanyika kwa njia ya mtandao na kuwashirikisha wabunge 121, wabunge 116 kati ya 217 wamepitisha rasimu ya sheria inayofuta hatua za dharura zilizotangazwa na Rais Saied Julai 25 mwaka jana, ambazo ni pamoja na kuivunja serikali na kusimamisha kazi ya Bunge. Wapinzani wake walizitaja hatua hizo kuwa ni mapinduzi dhidi ya Katiba na dhidi ya mapinduzi ya wananchi yaliyouondoa madarakani utawala wa dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Zine El Abidine Ben Ali.

Miezi kadhaa iiliyopita Rais Kais Saied wa Tunisia alichukua uamuzi wa ghafla na wa kushangaza wa kusitisha shughuli za Bunge na kuwafuta kazi Spika na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, na kisha akatwaa udhibiti wa masuala yote ya utendaji nchini humo.