Mar 31, 2022 10:30 UTC
  • Wamorocco waandamana kuwaunga mkono Wapalestina

Wananchi wa Morocco wamefanya maandamano mbele ya Bunge la nchi hiyo huko Rabat na katika miji mingine kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Ardhi na kuonyesha mshikamano wao kwa wananchi wa Palestina.

Tarehe 30 mwezi Machi kila mwaka huadhimishwa huko Palestina kama "Siku ya Ardhi".

Kuainishwa siku hiyo kunahusiana na matukio yaliyojiri Palestina mwaka 1976; siku ambayo wazayuni maghasibu walipora na kuhodhi sehemu kubwa ya ardhi za Wapalestina. Katika kubainisha hisia na malalamiko yao dhidi ya unyang'anyi huo, wananchi wa Palestina waliandamana, lakini kadhaa miongoni mwa waliuawa shahidi na wengine wengi walijeruhiwa.

Katika upande mwingine, hatua ya Morocco ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni mwishoni mwa mwaka juzi wa 2020 imeendelea kupingwa na kukosolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na makundi mbalimbali ya nchini humo. 

Wananchi wa Morocco jana Jumatano Machi 30 kwa mara nyingine tena walitangaza upinzani wao dhidi ya kitendo cha nchi za Kiarabu, ikiwemo Morocco, kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel. Wananchi wa Morocco wamefanya maandamano hayo wakiitikia wito uliotolewa na kundi la " the National Action Group for Palestine in Morocco." 

Miji ya Rabat, Casablanca, Beni Mellal, Meknes, Berkane, Tetouan, Marrakeshi, Fez Bejaad na Mohammedia ilishuhdia maandamano hayo ya maadhimisho ya "Siku ya Ardhi" yaliyoshirikisha wanaharakati wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu. 

Kwa mnasaba wa Siku ya Ardhi, Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina (PCBS) imetangaza kuwa utawala haramu wa Israel hivi sasa umehodhi zaidi ya asilimia 85 ya ardhi ya nchi hiyo kulingana na mipaka ya kihistoria.

Tags