Msomali aliyefanya jinai za kivita anafanya kazi uwanja wa ndege Marekani
Imearifiwa kuwa, mtuhumiwa wa jinai za kivita raia wa Somalia anafanya kazi katika uwanja wa ndege wa kimataifa katika mji wa Washington D.C nchini Marekani.
Kanali ya televisheni ya Press TV ya Iran imenukuu Shirika la habari la CNN lililoripoti kuwa, Yusuf Abdi Ali ni mlinzi katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Dulles mjini Washington kwa muda wa miaka sita sasa, licha ya kukabiliwa na mashitaka ya kutenda jinai za kivita nchini Somalia miaka ya 80. Habari zinasema kuwa, Yusuf Abdi Ali alikuwa kamanda mwandamizi wa jeshi la Somalia wakati watu wa jamii ya Isaaq walipotendewa jinai za kutisha na wanajeshi wa Kisomali katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Idadi kubwa ya watu wa jamii hiyo waliuawa na wanajeshi wa Somalia na kuzikwa katika makaburi ya umati mbali na wengine wengi kukandamizwa na kudhalilishwa.
Kamanda huyo wa zamani wa jeshi la Somalia alitorokea Canada baada ya kuanguka kwa serikali ya kidikteta ya Siad Barre mwaka 1991. Baadaye aliingia Marekani kwa kutumia viza ya mkewe Intisar Farah, ambaye alipewa uraia na Marekani alipodai kuwa anatoka jamii ya Waisaaq nchini Somalia.
Kwa mujibu wa Kathy Roberts, wakili katika shirika la kutetea haki za binadamu la Center for Justice and Accountability, kuna takriban watuhumiwa 1,000 wa jinai za kivita kutoka nchi mbali mbali wanaoishi nchini Marekani.