Jun 11, 2022 11:18 UTC
  • Ajali za barabarani zaua watu 25 Tanzania ndani ya saa 24

Watu watano wamepoteza maisha na wengine tisa wamejeruhiwa baada ya basi dogo aina ya Coaster waliyokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka nchini Tanzania.

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Kalisti Lazaro amesema ajali hiyo ilitokea jana Ijumaa Juni 10 katika kijiji cha Mbaramo Tarafa ya Umba wilayani humo.

Lazaro amesema gari hilo lilikuwa linarejea Dar es Salaam kutoka msibani katika kijiji cha Mbaramo. Amesema majeruhi sita wamepelekwa katika Hospital ya Rufaa ya Bombo mkoani Tanga, huku watatu wakiwa wanaendelea kupata matibabu katika Kituo cha Afya cha Mnazi kilichopo wilayani Lushoto.

Haya yanaripotiwa katika hali ambayo, idadi ya watu waliofariki dunia kwenye ajali nyingine ya jana Ijumaa iliyohusisha basi dogo la Coaster kugongana na lori lililokuwa limeharibika karibu na eneo la Changarawe, Mafinga mkoani Iringa imefikia 20.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema chanzo cha ajali hiyo iliyotokea jana ni uzembe wa dereva wa gari hilo lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda Mbeya.

Kuongezeka ajali za barabarani Tanzania

Amesema awali, dereva wa Coaster alipoteza mwelekeo na kuligonga lori ambalo lilikuwa limepata ajali kwenye eneo hilo. Ameeleza kuwa wakati abiria walionusurika wakiokoa majeruhi, lori jingine aina ya Volvo liliwagonga abiria waliokuwa wakiokolewa kwenye ajali ya kwanza na kusababisha vifo vingi zaidi.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, katika kila sekunde 24, mtu mmoja hufariki dunia kwenye ajali ya barabarani duniani, sawa na watu takribani watatu katika kila dakika moja na jumla ya watu 72 kila siku.

Tags