Khartoum yaituhumu Addis Ababa kuwanyonga wafungwa wa Sudan na kuonyesha miili yao
(last modified Tue, 28 Jun 2022 02:51:29 GMT )
Jun 28, 2022 02:51 UTC
  • Khartoum yaituhumu Addis Ababa kuwanyonga wafungwa wa Sudan na kuonyesha miili yao

Jeshi la Sudan limelitumu jeshi la Ethiopia kuwa limewanyonga wanajeshi 7 na raia mmoja wa Sudan waliokuwa wafungwa nchini humo, jambo ambalo limekanushwa na maafisa rasmi wa Ethiopia, wakieleza kuwa Addis Ababa itatoa tamko rasmi la kujibu madai hayo ya Sudan.

Baada tu ya kutolewa tuhuma hizo, Khartoum imemwita balozi wa Ethiopia nchini Sudan na kumsaili, na vilevile imemrejesha nyumbani balozi wake kutoka Addis Ababa kwa mashauriano.

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Sudan pia imetangaza kuwa imeanza kuwasilisha malalamiko yake katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa na ya kikanda dhidi ya Ethiopia, ikisisitiza kwamba "inalinda haki kamili iliyodhaminiwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa ya kutetea ardhi yake na hadhi ya taifa hilo."

Jeshi la Sudan limeashiria - katika taarifa yake - kwamba Ethiopia ilionesha miili ya watu waliouawa kwa umma, na kuahidi kwamba litajibu "hatua hii ya woga kwa namna inayofaa."

Duru za kijeshi za Sudan zimetangaza kuwa, Kamanda Mkuu wa Jeshi na Mkuu wa Baraza la Utawala, Abdel Fattah Al-Burhan, ametembelea eneo la Al-Fashqa la Sudan kwenye mpaka wa nchi hiyo na Ethiopia ili kujua athari za tukio hilo.

Ni muhimu kukumbusha kuwa mpaka wa Sudan na Ethiopia umekuwa na mvutano kwa muda sasa, na Disemba 31 mwaka 2020 Sudan ilitangaza kwamba jeshi la nchi hiyo limechukua udhibiti wa ardhi zote zinazozozaniwa katika eneo la mpaka wa Al-Fashqa, huku Addis Ababa ikilishutumu jeshi la Sudan kuwa limevamia na kuteka kambi 9 ndani ya ardhi ya Ethiopia tangu Novemba 2021.

Tags