'Al-Shabaab' yaua mwanahabari wa kike mjini Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8566-'al_shabaab'_yaua_mwanahabari_wa_kike_mjini_mogadishu
Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wamemuua kwa kumfyatulia risasi mwandishi wa habari wa kike katika mji mkuu Mogadishu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 06, 2016 03:02 UTC
  • 'Al-Shabaab' yaua mwanahabari wa kike mjini Mogadishu

Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wamemuua kwa kumfyatulia risasi mwandishi wa habari wa kike katika mji mkuu Mogadishu.

Meja Nur Ali, ofisa wa ngazi za juu wa polisi mjini Mogadishu amesema kuwa, Sagal Salad Osman, mwandishi wa habari wa kituo cha redio cha serikali aliuawa jana Jumapili baada ya kufyatuliwa risasi na watu waliokuwa wamejizatiti kwa bunduki ambao walikimbia eneo la tukio baada ya kutekeleza ukatili huo. Kwa mujibu wa vuguvugu linalojiita Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari, wanahabari 45 wameuawa na watu wanaoaminika kuwa wanachama wa al-Shabaab tangu mwaka 2007, mbali na visa vya mauaji vya hivi karibuni ambavyo havijarekodiwa. Kulingana na takwimu za mwaka jana 2015 za Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka, Somalia ni nchi ya 172 kati ya 180 duniani, kwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.

Haya yanajiri siku chache baada ya vikosi vya usalama vya Somalia kumuua mkuu wa kitengo cha intelijinsia cha kundi la wanamgambo wa al-Shabaab anayejulikana kwa jina la Daud ambaye alikuwa akiliongoza tawi la kiitelijinsia la kundi hilo ambalo linajulikana kwa jina la "Amniyat". Hadi kufikia sasa al Shabaab haijatoa taarifa yoyote kuhusu mauaji hayo na kuuawa kwa mwanahabari huyo kunahesabiwa kuwa mwanzo wa hujuma zao za kulipiza kisasi. Itakumbukwa kuwa, Aprili mwaka huu, serikali ya Somalia ilitekeleza adhabu ya kifo dhidi ya mwanachama wa al-Shabaab aliyetoa amri na kufanikisha kuuawa wanahabari 6 wa Kisomali.