Wapinzani Tunisia waendelea kupinga katiba mpya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i87240-wapinzani_tunisia_waendelea_kupinga_katiba_mpya
Wakati Rais wa Tunisia Kais Saied ametangaza kutekelezwa kwa katiba mpya ya nchi, Harakati ya Ennahda ya Tunisia imepinga hatua hiyo na kusema katiba hiyo haina uhalali. Harakati ya Ennahda imetangaza katiba mpya kama jaribio la kuhalalisha mapinduzi dhidi ya katiba, na pia ni dhidi ya mafanikio ya mwamko wa wananchi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 20, 2022 13:34 UTC
  • Wapinzani Tunisia waendelea kupinga katiba mpya

Wakati Rais wa Tunisia Kais Saied ametangaza kutekelezwa kwa katiba mpya ya nchi, Harakati ya Ennahda ya Tunisia imepinga hatua hiyo na kusema katiba hiyo haina uhalali. Harakati ya Ennahda imetangaza katiba mpya kama jaribio la kuhalalisha mapinduzi dhidi ya katiba, na pia ni dhidi ya mafanikio ya mwamko wa wananchi.

Katika katiba mpya ya Tunisia, ongezeko la mamlaka ya Kais Saied ni dhahiri kabisa. Kwa mujibu wa katiba mpya, rais atakuwa mkuu wa mhimili wa dola na pia uteuzi wa majaji utategemea idhini ya rais. Halikadhalika kwa mujibu wa katiba mpya ya Tunisia, mabunge mawili ya kutunga sheria yanayoitwa Baraza la Wawakilishi na Baraza la Kitaifa yataundwa nchini Tunisia, na sheria za mabunge haya mawili zitapitishwa tu ikiwa zitaidhinishwa na rais.

Suala la kubadilisha katiba ya Tunisia limesababisha mzozo mkubwa wa kisiasa nchini humo. Katika miezi kadhaa iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Tunisia,  Kais Saied, amechukua maamuzi kadhaa  ambayo hayajawaridhisha wengi hasa katika uga wa kisiasa nchini humo. Kuitisha kura ya maoni ya kubadilisha katiba imekuwa moja ya hatua ambazo zimeibua utata nchini humo.

Kura ya maoni ya marekebisho ya katiba ya Tunisia ilifanyika Julai 25 huku kukiwa na hali ya kutoridhika na maandamano ya wananchi na viongozi wa vyama vingi vya upinzani. Kura hiyo ya maoni ilisusiwa na makundi makubwa ya kisiasa na vyama vya nchi hii, kama vile Ennahda, Moyo wa Tunisia, Muungano wa Heshima, Harakati ya Irada na Matumaini ya Tunisia, Chama cha Republican, Harakati ya Demokrasia, Harakati ya Demokrasia ya Kazi na Uhuru, na Chama cha Leba.  Vyama hivyo vya upinzani vinasisitiza kuwa mchakato mzima wa mabadiliko ya katiba ulikiuka sheria.

Kulingana na ripoti ya Baraza la Uchaguzi la Tunisia, kiwango cha ushiriki katika kura ya maoni ya katiba mpya ya Tunisia kilitangazwa kuwa karibu 27%, ambayo ilikuwa uthibitisho wa kutoshiriki katika zoezi hilo ambalo liliitishwa na rais wa Tunisia.

Licha ya upinzani na kutoridhika kwa wananchi na vyama vya siasa, Rais  Kais Saied  alikaribisha matokeo ya kura ya maoni. Alizitaja kauli za wapinzani wa kura hii ya maoni kuwa ni za "uongo na zisizo na thamani".  Akieleza kuwa katiba mpya ni halali,  rais Saied ambaye ni mhadhiri na mtaalamu wa masuala ya sheria alisema kura ya maoni ya Julai 25 iliweza kuleta ufungamano kati  katiba na wananchi na hivyo  wale wanaojaribu kuchukua madaraka ya wananchi kwa lazima wawajibike kwa vyombo vya sheria.

Rais Saied amesema anaamini kwamba kwa kutekelezwa kwa katiba mpya, kutap[atikana njia sahihi katika mapinduzi na historia ya Tunisia.

Rais Kais Saied wa Tunisia

Licha ya kuanza kutekelezwa kwa katiba mpya, maandamano dhidi ya Rais Qais Saied yanaendelea. Wapinzani wanazingatia hatua yake kuwa ni  dhidi ya malengo ya mwamko wa wananchi mwaka  2011 na juhudi za kuanzisha demokrasia nchini Tunisia.

"Meytham Qassemi, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tunis, anasema kuhusiana na hili kwamba: "Demokrasia ya Tunisia kwa mara nyingine tena iko katika njia panda na hatari." Hatua ya Rais wa Tunisia kuidhinisha katiba mpya baada ya kura ya maoni iliyokumbwa na utata mkubwa inaonyesha kuwa nchi  kwa mara nyingine iko katika njia ya udikteta baada ya miaka kumi ya demokrasia ya kweli.

Chama cha Ennahda, kikiwa ni chama kikubwa na chenye ushawishi mkubwa nchini Tunisia, kilitangaza katika taarifa yake mpya kwamba katiba ya mpya haisuluhishi matatizo yoyote ya nchi, bali inaimarisha dhulma, msimamo wa upande mmoja.

Wanachama wa Ennahda wametoa wito kwa makundi yote yanayopinga katiba mpya kuunganisha juhudi zao za kukabiliana na kila kinachotajwa kuwa ni hatari ya udikteta na kufanya mazungumzo ya dharura ili kuibua misimamo ya pamoja itakayoinusuru nchi na hatari ya kuporomoka kwa uchumi na mlipuko wa kijamii.

Tunisia sasa iko katika hali ngumu ya kisiasa, kiasi kwamba baadhi ya watu wanaamini kuwa kile kitakacho jiri baada ya kufanyika kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba ni kurejea nchi hii katika zama za udikteta wa Ben Ali.

Shadi Hamid, mjumbe mkuu wa Taasisi ya Brookings, anasema kuhusiana na hili kwamba: Julai 25 ilikuwa siku ya kifo cha demokrasia ya Tunisia.

Pamoja na kwamba inaonekana kwa hali ilivyo sasa, juhudi za kufuta katiba mpya hazitafanikiwa, lakini juhudi za wananchi na vyama vya siasa katika nyanja hii zinaendelea.