Aug 25, 2022 12:04 UTC
  • DRC yafanya kampeni ya chanjo baada ya Ebola kuripotiwa Beni

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo Alkhamisi imezindua kampeni ya kutoa chanjo katika mji Beni, mashariki mwa nchi, baada ya kesi ya virusi hivyo kuthibitishwa katika mji huo.

Kesi mpya ya Ebola ilithibitishwa Jumatatu iliyopita na Wizara ya Afya ya DRC, katika jimbo la mashariki mwa nchi hiyo la Kivu Kaskazini.

Mwanamke mwenye umri wa miaka 46 alifariki dunia tarehe 15 Agosti 2022 huko Beni, mji ulioko Kivu Kaskazini. Mgonjwa huyo alipata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Beni, awali kwa ajili ya magonjwa mengine, lakini baadaye, ilionyesha dalili zinazoambatana na ugonjwa wa virusi vya Ebola.

Vipimo vilivyofanywa na taasisi ya National Institute for Biomedical Research mjini Goma vilithibitisha kuwa kesi hiyo ni ya spishi ya Zaire.

Spishi hiyo inahusishwa na mripuko wa 10 wa ugonjwa wa Ebola nchini DRC, ulioripotiwa katika mikoa ya Ituri na North Kivu kuanzia mwaka 2018 hadi 2020, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 2,000.

Maiti ya mgonjwa wa Ebola

Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita wa Julai, Shirika la Afya Duniani WHO lilitangaza kuwa, mripuko wa Ebola uliotangazwa tarehe 23 mwezi Aprili mwaka huu huko Mbandaka, mji mkuu wa jimbo la Equateur katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umetokomezwa.

Ikumbukwe kuwa, mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa hatari wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika. 

Tags