Gambia kuimarisha hatua za kiafya kufuatia vifo vya watoto 66
(last modified Sun, 09 Oct 2022 02:56:32 GMT )
Oct 09, 2022 02:56 UTC
  • Gambia kuimarisha hatua za kiafya kufuatia vifo vya watoto 66

Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Rais Adama Barrow wa Gambia ameeleza kuwa nchi hiyo itaimarisha hatua za kiafya ikiwa ni pamoja kudhibiti ubora wa dawa kutoka nje baada ya vifo vya kustaajabisha vya makumi ya watu nchini humo.

Akiwahutubia wananchi, Rais wa Gambia amesema kuwa: nawahakikishia wote kwamba serikali haitaacha lolote ili kubaini ukweli katika tukio hili”. Amesema, Wizaraya Afya  tayari imeanzisha uchunguzi kuhusu chanzo cha dawa hizo zenye viambata sumu, mazingira na taratibu za uingizaji wa dawa nchini na kuweka ulinzi wa kutokomeza uingizaji wa dawa zisizo na viwango huko Gambia”.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Gambia imezindua kampeni ya dharura ya nyumba kwa nyumba ya kukusanya dawa za kikohozi na mafua zinazodaiwa kuwa chanzo cha vifo vya watoto 66 wa nchi hiyo baada ya kusababisha madhara kwa figo za watoto  na hatimaye kushindwa kabisa kufanya kazi miezi mitatu iliyopita. 

Rais Adama Barrow wa Gambia amesema kuwa mlipuko wa vifo vya watoto nchini humo sasa umedhibitiwa, huku kukiwa na kesi mbili tu zilizoripotiwa wiki mbili za karibuni. Jumatano iliyopita Shirika la Afya Duniani lilitoa tahaddhari kuhusu dawa nne za maji za kutibu kikohozi na mafua zilizotengenezwa na Kampuni ya dawa ya Maiden Pharmaceuticals ya India juu ya uwezekano wa kuwa ndizo zilizosababisha vifo vya watoto huko Gambia. WHO aidha inaendelea kuichunguza kampuni hiyo na mamlaka za udhibiti wa viwango na ubora wa bidhaa za India.

Dawa zinazodaiwa kusababisha vifo vya watoto 66 nchini Gambia