Maiti 230 zagunduliwa katika makaburi ya umati Libya
Mamlaka za Libya zimetangaza habari ya kugunduliwa miili 230 ya watu wasiojulikana katika makaburi ya umati katika mji wa Tarhuna, ulioko kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.
Hayo yametangazwa na Karim Asad Ahmad Khan, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), katika waraka wake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kuitembelea Libya.
Ushahidi na vielelezo vya mikanda ya video na sauti vilivyokusanywa na Karim Khan katika ziara yake hiyo nchini Libya vimeonyesha kuwa, vikosi vitiifu kwa Khalifa Haftar, mbabe wa kivita na jenerali muasi wa Libya vimehusika na mauaji na ukatili wa kuchupa mipaka katika miji kadhaa ya Libya, ukiwemo mji wa Tarhauna.
Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya ICC ametoa mwito wa kuchunguzwa Haftar na wapiganaji wanaomuunga mkono, kwa kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu nchini Libya.

Mwezi uliopita wa Oktoba pia, mamlaka za Libya zilitangaza kupatikana kwa miili 42 ambayo haikutambuliwa katika kaburi la pamoja huko Sirte, makao makuu ya zamani ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).
Aidha mwezi Agosti mwaka huu, makaburi mawili ya halaiki yenye miili saba na minane mtawalia, yaligunduliwa katika ua wa hospitali moja huko huko Sirte, yapata kilomita 450 mashariki mwa Tripoli.
Tangu kupinduliwa na kuuliwa kwa Muammar Gaddafi mwaka 2011, Libya bado inatawaliwa na ukosefu wa amani na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyochochewa na uingiliaji wa nchi za kigeni.