Dec 02, 2022 10:57 UTC
  •  Cyril Ramaphosa
    Cyril Ramaphosa

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini anakabiliwa na miito mbalimbali inayomtaka ajiuzulu baada ya uchunguzi wa Bunge kubaini kuwa huweda alikiuka sheria za kupambana na ufisadi kuhusiana na wizi wa mamilioni ya dola katika shamba lake la Phala Phala.

Haya yameelezwa kufuatia madai yaliyowasilishwa na Arthur Fraser, Mkuu wa zamani wa Intelijinsia wa Afrika Kusini kwamba, Rais Cyril Ramaphosa alijaribu kuficha wizi wa mamilioni ya dola shambani kwake mwaka 2020. 

Ramaphosa alitazamiwa kufika bungeni jana kujibu maswali, hata hivyo kikao kiliakhirishwa. Dr. Dale T.McKinley mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Ushahidi unaonekana kuwa mwingi katika kashfa hiyo inayomkabili Ramaphosa. Amesema, Ramaphosa amelifanya suala hilo kuwa la siri sana na kuficha mambo, jambo ambalo litaharibu kabisa uhalali wake wa kisiasa.

Kamati ya uchunguzi ya Bunge la Afrika Kusini iliibua maswali katika ripoti yake kuhusu chanzo cha fedha hizo za Cyril Ramaphosa na kwa nini kiasi chote hicho hakikutangazwa kwa mamlaka husika za fedha. Rais wa Afrika Kusini kwa upande wake amekanusha tuhuma za ufisadi dhidi yake na kusema alizipata kutokana na mauzo ya wanyama wa shambani kwake. Wakati huo huo, vyama vya upinzani na wapinzani wa Ramaphosa ndani ya chama tawala cha ANC vimetoa wito wa kujiuzulu Ramaphosa. 

Maandamano ya kushinikiza kujizulu Rais wa Afrika Kusini 

Sarafu ya Afrika Kusini imeshuka thamani kutokana na kashfa hiyo inayoendelea dhidi ya Rais wa nchi hiyo. Wabunge wa Afrika Kusini wanatazamiwa kujadili ripoti iliyowasilishwa bungeni Jumanne ijayo ambapo watapiga kura iwapo hatua zinapasa kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuendelea na mchakato wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Ramaphosa au la.  

Tags