Boko Haram waua watu 4 na kuteka nyara wanawake 3 Chibok, Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9259-boko_haram_waua_watu_4_na_kuteka_nyara_wanawake_3_chibok_nigeria
Wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram wameua wanakijiji wasiopungua wanne na kuwateka nyara wanawake watatu karibu na mji wa Chibok ulioko kaskazini mashariki mwa Nigeria ambako miaka miwili nyuma waliwateka nyara wasichana zaidi ya 200.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 15, 2016 15:36 UTC
  • Boko Haram waua watu 4 na kuteka nyara wanawake 3 Chibok, Nigeria

Wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram wameua wanakijiji wasiopungua wanne na kuwateka nyara wanawake watatu karibu na mji wa Chibok ulioko kaskazini mashariki mwa Nigeria ambako miaka miwili nyuma waliwateka nyara wasichana zaidi ya 200.

Wakaazi na manusura wa tukio wamesema, magaidi wa kundi hilo la kitakfiri jana alfajiri walishambulia kijiji cha Kautuva, wakazichoma moto nyumba na kuwafyatulia risasi wakaazi wa kijiji hicho.

Ali Pangu, mmoja wa wanamgambo wa sungusungu wanaoshirikiana na jeshi la Nigeria kupambana na kundi hilo la kigaidi amesema baadhi yao walikuwa na bahati kwa kunusurika na mauaji na wakaweza kukimbilia mjini Chibok.

Mkaazi mwengine wa kijiji hicho amesema, magaidi wa kundi la Boko Haram waliwateka nyara pia wanawake watatu.

Kijiji cha Kautuva kiko karibu na mji wa Chibok ambao mnamo mwezi Aprili mwaka 2014 ulivamiwa na wanamgambo wa Boko Haram na kutekwa nyara wasichana 276 wanafunzi wa shule moja ya mji huo.

Uasi na mashambulio ya kigaidi ya kundi la Boko Haram yanayoendelea kwa mwaka wa saba sasa yameshasababisha vifo vya watu wapatao 15,000 na kuwaacha wengine zaidi ya milioni mbili wakibaki bila ya makaazi.

Chini ya uongozi wa Rais wa sasa wa Nigeria Muhammadu Buhari na kwa msaada wa nchi jirani, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuyakomboa karibu maeneo yote yaliyokuwa yakishikiliwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, hata hivyo kundi hilo lingali linaendelea kufanya mashambulio ya uripuaji mabomu kwa kutumia washambuliaji wa kujitoa mhanga.../