Feb 04, 2023 13:23 UTC
  • Viongozi wa Afrika Mashariki wako Burundi kujadili machafuko ya Congo DR

Viongozi wa nchi za Afrika Mashariki wamewasili nchini Burundi leo Jumamosi kwa mkutano wa kanda kujadili mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokfrasia ya Congo.

Mkutano huo unafanyika katika mji wa Bujumbura ambao ni kitovu cha kuchumi cha Burundi chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo inaongoza juhudi za upatanishi ili kumaliza mapigano mashariki mwa taifa hilo kubwa la Afrika ya kati.

Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki imesema: "Ajenda ya mkutano wa dharura wa Bujumbura ni kutathmini hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo."

Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye anatuhumiwa kuunga mkono makundi ya waasi mashariki mwa DRC, ni miongoni mwa viongozi wa EAC wanaohudhuria mkutano wa Bujumbura-- ikiwa ni ziara yake ya kwanza nchini Burundi tangu 2013 alipohudhuria sherehe za uhuru wa nchi hiyo.

Majirani hao wawili katika eneo la Maziwa Makuu ya Afrika, kwa muda mrefu wamekuwa na uhusiano wenye misukosuko, kila mmoja akimshutumu mwenzake kuwa anaingilia masuala yake ya ndani.

Tshisekedi na Kagame

Mwaka 2020, Rais Paul Kagame wa Rwanda alimtaka rais aliyekuwa amechaguliwa wakati huo wa Burundi, Evariste Ndayishimiye kurejesha uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande mbili lakini wito wake ulikataliwa na kutajwa kuwa ni wa "kinafiki".

Marais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, William Ruto wa Kenya, Felix Tshisekedi wa Congo DR, Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda walikuwa tayari wamewasili mjini Bujumbura kushiriki katika mkutano huo. 

Tags