Apr 25, 2024 10:17 UTC
  • UN: Hali mashariki mwa DRC inatisha na kuna hatari ya mzozo kusambaa kikanda

Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Kanda ya Maziwa Makuu amewasilisha kwa Baraza la Usalama taswira ya kutisha ya hali ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, inayoambatana na mvutano unaoendelea kati ya nchi hiyo na Rwanda, na hatari ya mzozo huo kusambaa kikanda.

Huang Xia amewasilisha tarifa yake mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama na kusema: "mvutano kati ya DRC na Rwanda sio tu unaendelea, lakini pia umechangiwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya wapiganaji wa kundi la M23 na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo FARDC." 

Katika tarifa hiyo Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Kanda ya Maziwa Makuu amesema anatiwa wasiwasi  na ukubwa wa hali hiyo, inayogubikwa hasa na kuongezeka kwa machafuko na kuzorota kunakotia wasiwasi kwa hali ya kibinadamu mashariki mwa DRC. 

Xia ameendelea kusema: "kilichoongezwa kwa hili ni kuendelea kwa kauli za malumbano kati ya DRC na Rwanda huku kukiwa na shutuma zinazofanana za mipango ya kuvuruga utulivu na kuzuka kwa kauli za chuki." 

Rais Paul Kagame wa Rwanda (kulia) na Rais Felix Tshisekedi wa DRC

Mwanadiplomasia huyo wa UN amebainisha kuwa, zaidi ya hayo, mvutano kati ya Burundi na Rwanda, unaohusishwa kwa karibu na hali ya mashariki mwa DRC, unazidisha hali ya wasiwasi na kuathiri maendeleo makubwa yaliyorekodiwa tangu 2020 katika uhusiano kati ya nchi hizi mbili.

Katika muktadha huo wa kutisha, mjumbe wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba ni muhimu "kuongeza haraka juhudi za kupunguza mvutano, ili kuepusha moto wa kikanda na kwamba hii ili isitokee ni lazima iwe kwa njia ya mazungumzo ya wazi na ya dhati kati ya pande zinazohusika".

Vilevile amepongeza juhudi za kisiasa na kidiplomasia za viongozi kadhaa wa Afrika na washirika wa kimataifa kutafuta suluhu ya mgogoro huo…/

 

 

 

 

Tags