UN yaikosoa Tunisia kwa kuwawekea mbinyo wakosoaji na wapinzani
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa umoja huo unatiwa wasiwasi na kushtadi wimbi la kamatakamata dhidi ya wanaharakati wa kisiasa na wapinzani wa serikali ya Rais Kais Saeid wa Tunisia.
Volker Tukr amesema Umoja wa Mataifa umesikitishwa na vitendo hivyo vya kukamatwa kiholela wanaharakati wa kisiasa na wapinzani wa serikali ya Rais Kais Saeid wa Tunisia.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Ofisi Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, kwa akali watu tisa wametiwa mbaroni katika wimbi hilo jipya la kamatakamata huko Tunisia, baadhi ya wakikabiliwa na mashitaka ya ufisadi na wengine uhujumu wa usalama.
Vyombo vya habari vya Tunisia vimesema baadhi ya watu waliotiwa mbaroni hivi karibuni ni majaji wawili wa zamani, wakili, mfanyabiashara mashuhuri na baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa, kikiwemo cha Ennahdha.
Haya yanajiri wakati huu ambapo maafisa usalama wa Tunisia wameshadidisha wimbi hilo la kuwatia nguvuni wanaharakati wa kisiasa wa nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Hivi karibuni, Rashed Al-Ghannoushi, kiongozi wa Vuguvugu la Ennahdha la Tunisia, alitoa taarifa ya kulaani kukamatwa Nouruddin Al-Bahiri, mmoja wa wanachama waandamizi wa vuguvugu hilo na Nouruddin Butar, mkurugenzi wa kituo cha redio cha Mosaic FM.
Muungano mkuu wa upinzani Tunisia unaokijumuisha chama cha Kiislamu cha Ennahdha umesisitiza udharura wa kuweko umoja na mshikamano dhidi ya Rais wa nchi hiyo, Kais Saied.