Mali: Russia ni mshirika wa kutegemewa wa nchi za Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i94570-mali_russia_ni_mshirika_wa_kutegemewa_wa_nchi_za_afrika
Kaimu Waziri Mkuu wa Mali amesema Russia inaliheshimu na imelisaidia pakubwa taifa hilo la Afrika Magharibi katika vita dhidi ya ugaidi, na imethibitisha kivitendo kuwa haina masharti wala malengo fiche kwenye usaidizi wake.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Feb 28, 2023 22:50 UTC
  • Mali: Russia ni mshirika wa kutegemewa wa nchi za Afrika

Kaimu Waziri Mkuu wa Mali amesema Russia inaliheshimu na imelisaidia pakubwa taifa hilo la Afrika Magharibi katika vita dhidi ya ugaidi, na imethibitisha kivitendo kuwa haina masharti wala malengo fiche kwenye usaidizi wake.

Choguel Kokalla Maiga amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la RIA Novosti na kueleza kuwa, kwa msaada kijeshi wa Russia, hivi sasa magaidi hawawashtui tena wananchi wa Mali, bali magenge ya kigaidi ndiyo yanatiwa kiwewe na jeshi la nchi hiyo.

Maiga ameeleza bayana kuwa, Russia ni rafiki na mshirika wa kutegemewa kwa Mali na mataifa mengine ya Afrika, na wala haina undumakuwili na nyuso mbili kwenye misimamo na sera zake.

Kaimu Waziri Mkuu wa Mali amesema misaada ya Russia kwa taifa hilo haishii tu kwenye silaha na zana za kijeshi, lakini pia katika masuala ya kibinadamu kama misaada ya chakula, mbolea, na nishati. 

Maiga amesema, "Hatutaki kuwa mateka wa mataifa mengine, ambayo mpaka yafanye maamuzi ya kutupa au kutotupa fueli na kuweka chakula kwenye meza ya wananchi wa Mali."

Wanajeshi wa Mali

Kadhalika amekosoa mitazamo ya Umoja wa Ulaya kwa taifa hilo la Afrika Magharibi, na haswa matamshi ya hivi karibuni ya Charles Michel, Rais wa Baraza la Ulaya. Michel mapema Februari alikiambia kituo kimoja cha habari cha Ufaransa kuwa, Bamako imefanya makosa kwa kuvunja uhusiano na washiriki wake wa 'asili' haswa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Mali amesema kauli hiyo ya Rais wa Baraza la Ulaya ni muendelezo wa kampeni yao ya upotoshaji. Amekariri kauli yake ya huko nyuma kuwa, Ufaransa ndiyo sababu ya matatizo mbalimbali ya kiusalama na kiuchumi yanaoisumbua nchi hiyo ya Afrika Magharibi.