UNHCR yatahadharisha kuhusu mgogoro wa binadamu Somaliland, maelfu wanakimbilia Ethiopia
Karibu watu laki moja wanaokimbia mapigano huko Somaliland; eneo lililojitenga kaskazini mwa Somalia, kwa muda wa mwezi mmoja sasa wamepewa hifadhi katika eneo moja nchini Ethiopia. Raia hao wa Somaliland wamekimbia huko licha ya eneo hilo kuathiriwa na ukame mkubwa. Hayo yameelezwa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR).
Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa inakadiria kuwa watu 98,000 wamewasili katika wilaya tatu huko Ethiopia zinazopakana na eneo la Somaliland tangu Februari 6 mwaka huu.
Tesfahun Gobezay Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Wakimbizi na Raia Wanaorejea Makwao (RRS), taasisi inayosimamiwa na serikali ya Ethiopia, amesema katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa nchi hiyo, Addis Ababa akiwa pamoja na Mamadou Dian Balde Mwakilishi Mkazi wa UNHCR nchini Ethiopia kwamba: Taasisi hiyo itathibitisha idadi hiyo ya wakimbizi kwa usajili ambao umeanza."
Wimbi hilo la wakimbizi wa Somaliland kuelekea Ethiopia linashuhudiwa kufuatia mvutano ulioibuka katika miezi ya hivi karibuni na kusababisha mapigano kati ya vikosi vya Somaliland na vikundi vinavyoitii serikali ya Somalia, haswa katika eneo la Las Anod.

Takwimu za hadi kufikia Jumatatu wiki hii zinazonyesha kuwa wakimbizi 29,000 raia kutoka Somaliland tayari wamejiandikisha katika wilaya hizo tatu huko Ethiopia na bado wanaongezeka. Aghlabu ya wakimbizi hao ni wanawake na watoto.
Mamadou Dian Balde Mwakilishi Mkazi wa UNHCR nchini Ethiopia amesisitiza kuwa mambo mengi kama makazi, chakula, maji na huduma za matibabu yanahitajika; na yote hayo ni masuala ya dharura sana. Amesema, misaada hiyo yote inapasa pia kuwazingatia wenyeji wanaowapokea wakimbizi na si wakimbizi pekee yao.
Eneo la Somaliland hapo awali lilikuwa chini ya utawala wa Uingereza, kabla ya kutangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991, katika hatua ambayo haijatambuliwa na jamii ya kimataifa.