Apr 14, 2023 02:28 UTC
  • Watu 24 wauawa katika mapigano ya kikabila Darfur, Sudan

Serikali ya Sudan imetangaza kuwa itachukua hatua kuunda jimbo jipya huko Darfur magharibi mwa nchi hiyo fikapo mwishoni mwa mwaka huu; eneo linalopakana na Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mohammed Hussein Timane Mjumbe wa Baraza la Foro Baranga, mji unaopatikana katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan umbali wa kilomita 185 kutoka makao makuu ya mji huo ya Al-Geneina ameeleza kuwa, tokea Jumamosi iliyopita hadi sasa kumeripotiwa vifo vya watu 24 vilivyotokea katika mapigano ya kikabila jimboni humo. 

Jumatatu wiki hii maafisa wa serikali za mitaa walitangaza amri ya kafyu ya usiku na hali ya hatari huko Darfur kwa muda wa mwezi mmoja. Mohammed Hussein Timane ameongeza kuwa, hali ya utulivu imerejea kwa kiwango fulani hata hiyo askari usalama bado wapo katika mji wa Foro Baranga mahali palipojiri mapigano.

Umoja wa Mataifa aidha umeripoti kuwa nyumba 50 zimechomwa moto huko Foro Baranga na familia zisizopungua 4,000 au watu 20,000 wamehama makazi yao. Jimbo la Darfur huko magharibi mwa Sudan mara kwa mara limekuwa likikumbwa na mapigano ya kikabila ambayo husababishwa na mambo mbalimbali miongoni mwake ikiwa ni mizozo ya ardhi na ugumu wa kupata huduma ya maji. 

Jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan 

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, vita vya ndani vilivyotokea Sudan mwaka 2003 kati ya utawala wa wakati huo wa Omar Hassan al Bashir na makundi ya uasi kutoka makabila ya waliowachache yalisababisha kuuliwa watu laki tatu na kupelekea wengine wanaokaribia milioni 2.5 kuwa wakimbizi.

 

Tags