Mar 02, 2024 03:08 UTC
  • Ripoti ya UN: RSF inashambulia na kuua raia Darfur, Sudan kwa msingi wa ukabila

Ripoti mpya ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imesema, Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF pamoja na wanamgambo vinaoshirikiana nao wanaopigania kutwaa madaraka nchini Sudan wamefanya mauaji ya kikabila na ubakaji wakati wa udhibiti wa eneo kubwa la Darfur magharibi mwa nchi hiyo, na kwamba vitendo hivyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, inatoa picha ya kutisha ya ukatili uliofanywa na RSF dhidi ya Waafrika huko Darfur.
 
Aidha, inaeleza jinsi vikosi vya usaidizi wa haraka vilivyofanikiwa kuyadhibiti majimbo manne kati ya matano ya Darfur, ikiwa ni pamoja na kwa kutumia mitandao tata ya kifedha inayohusisha makampuni kadhaa.
 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Jopo la wataalamu wa UN, Darfur inakabiliwa na "machafuko mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu 2005."
 
Sudan ilitumbukia katika machafuko mwezi Aprili mwaka jana, wakati mvutano wa muda mrefu kati ya jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan, na wanamgambo wa RSF wakiongozwa na Mohammed Hamdan Dagalo, ulipozusha mapigano ya mitaani katika mji mkuu, Khartoum.

Mapigano hayo yameenea katika maeneo mengine ya nchi, lakini yamechukua sura tofauti katika jimbo la Darfur, ambako wanamgambo wa RSF wamefanya mashambulizi ya kikatili dhidi ya raia Waafrika, hasa wa kabila la Masalit.

Miongo miwili iliyopita, Darfur ilijulikana kwa mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita, hasa uliofanywa na wanamgambo maaarufu wa Janjaweed dhidi ya watu wanaotambuliwa kama Waafrika wa Kati au Mashariki.

Inavyoonekana, hali ileile ya wakati huo imerejea tena, kiasi kwamba Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC Karim Khan alitangaza mwishoni mwa Januari kwamba, kuna sababu za kuamini kuwa pande zote mbili zinazopigana nchini Sudan zinafanya uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu au mauaji ya kimbari huko Darfur.

Mzozo unaoendelea nchini Sudan umesababisha hali mbaya sana ya kibinadamu na kupelekea watu wapatao milioni sita na laki nane kuyahama makazi yao, milioni tano na laki nne wakibaki bila makazi ndani ya nchi hiyo na milioni moja na laki nne ambao wamekimbilia nchi nyingine, wakiwemo laki tano na nusu waliotafuta hifadhi katika nchi jirani ya Chad.../

Tags