Apr 15, 2023 02:23 UTC
  • Indhari kuhusu magonjwa yanayotokana na maji Somalia baada ya mvua kubwa

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeonya kwamba mafuriko ya ghafla yaliiyotokea Somalia yanaweza kusababisha milipuko ya magonjwa yanayotokana na maji.

Ofisi hiyo imesema, mvua kubwa zilizonyesha Somalia zimekuja huku mlipuko wa kipindupindu na kuhara umeripotiwa katika mkoa wa Jubaland, kusini mwa Somalia, na mkoa wa Kusini Magharibi.

Ikinukuu takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya ya Somalia, OCHA imesema karibu kesi 4000 zinazoshukiwa kuwa na kipindupindu na vifo 17 vinavyohusishwa na ugonjwa huo vimeripotiwa katika wilaya 27 nchini humo tangu mwezi Januari.

OCHA imesema, maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko ni wilaya ya Bardhere mkoani Gedo, kusini mwa Somalia, na wilaya ya Baidoa iliyoko mkoa wa Bay, kusini magharibi mwa Somalia.

Msimu wa Gu (mvua) Somalia kawaida huanzia Aprili hadi Juni.

OCHA imeonya kuwa, "Ikiwa mvua kubwa itaendelea kunyesha nchini Somalia na katika nyanda za juu za Ethiopia katika msimu huu, inakadiriwa kuwa mafuriko ya ghafla yanaweza kuathiri hadi watu milioni 1.6, na zaidi ya 600,000 wanaweza kukimbia makazi yao.

Mafuriko nchini Somalia

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa  limesema kuwa watu wengi watakaokimbia makazi yao ni wale walio kwenye maeneo ya kando ya mito ya Juba na Shabelle, na sehemu za mikoa ya Bay na Banadir na pia huko Galmudug, Puntland na eneo lililojitangazia uhuru la Somaliland.

OCHA imesema zaidi ya watu 21 walikufa kutokana na mafuriko katika wilaya ya Bardhere, Jimbo la Jubaland, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kuanzia Machi 21 hadi 24.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linasema mvua kubwa zilizoandamana na mafuriko zimekuja kufuatia misimu mitano ya ukame ambayo imesababisha zaidi ya Wasomali milioni 1.4 kuhama makazi yao na kuua mifugo milioni 3.8 tangu katikati ya 2021.

Tags