Mkuu wa upinzani Kongo DR ahukumiwa miaka 3 jela
Mahakama moja katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imemhukumu miaka mitatu jela, kinara wa upinzani nchini humo ambaye pia ni mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu ujao, Moise Katumbi, aliyekuwa anakabiliwa na tuhuma za mauzo ya nyumba kinyume cha sheria.
Mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo mjini Lubumbashi katika mkoa wa Haut-Katanga, kusini mashariki mwa Kongo DR aliiambia mahakama hiyo jana Jumatano kuwa, Katumbi amefanya uporaji wa nyumba ya raia wa Ubelgiji ajulikanaye kwa jina la Alexandros Stoupis na baadaye kuiuza. Hata hivyo mawakili wa Moise Katumbi hawakupewa nafasi ya kumtetea mteja wao ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi. Moise Katumbi alisafiri barani Ulaya kwa ajili ya matibabu karibu mwezi mmoja sasa. Mwezi mmoja uliopita, mwendesha mashtaka mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alimruhusu mwanasiasa huyo aende Afrika Kusini kwa matibabu, ambapo baadaye alielekea barani Ulaya kwa matibabu zaidi. Mbali na tuhuma hizo za uporaji wa nyumba, serikali ya Rais Joseph Kabila inadai kuwa ina nyaraka na ushahidi unaoonesha kuwa, Meya huyo wa zamani wa Katanga alihusika katika kusajili mamluki wa kigeni wakiwemo askari kadhaa wa Kimarekani waliostaafu kwa lengo la kutekeleza njama dhidi ya taifa. Wafuasi wake wanasema kuwa, tangu kiongozi wao huyo ambaye ni mmiliki wa klabu maarufuku ya soka ya TP Mazembe atangaze nia yake hiyo ya kuwania kiti cha urais amekuwa akiandamwa na serikali ya Kinshasa kila uchao.