Ethiopia yawatimua Waganda waliohadaiwa kwenda 'kuonana' na Yesu
Mamlaka za Ethiopia zimewarejesha nyumbani raia 80 wa Uganda ambao walitapeliwa fedha zao kwa ahadi kwamba watapelekwa kukutana na Yesu katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uganda, Simon Peter Mundeyi amesema baada ya kundi hilo la waumini wa Kikristo kuwasili Ethiopia, waliviambia vyombo vya usalama nchini humo kwamba wamesafiri kwenda kukutana na Yesu Kristo, kama walivyoahidiwa na mchungaji wao, Pasta Simon Opolot wa Kanisa la Christ Disciples lililoko Soroti, mashariki mwa Uganda.
Kiongozi huyo wa kidini amekuwa akisakwa na maafisa usalama wa Uganda, akikabiliwa na tuhuma za kuwashawishi wafuasi wa kanisa hilo wauze mali zao ili wajiandae kukutana na Yesu.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda, wafuasi hao waliamriwa wajizuie kula chakula kwa siku 40, na kisha waelekee Ethiopia siku ya 41 ili wakakutane na Yesu Masihi nchini Ethiopia.
Wakati huohuo, maafisa wa upelelezi wa Kenya wamepata miili kumi zaidi kutoka kwenye makaburi ya halaiki katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifu unaohusishwa na ibada ya kufunga hadi kufa kwa ajili ya kwenda kukutana na Yesu mbinguni, na kufanya idadi ya waliofariki dunia hadi jana kufikia 284.
Aidha idadi ya watu waliotoweka walioripotiwa kuwa waumini wa kanisa la Good News International la mchungaji Paul Mackenzie ni takriban 613. Waliokolewa kufikia sasa ni 95. Ufukuzi wa maiti zaidi katika eneo hilo unaendelea hii leo.