Uganda yawatia mbaroni watu 20 wanaoshukiwa kushiriki katika mauaji ya kutisha shuleni
Polisi ya Uganda imeeleza kuwa imewatia mbaroni watu 20 kwa tuhuma za kushirikiana na wanamgambo wa kundi la ADF wanaodaiwa kushambulia shule moja karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumamosi iliyopita.
Msemaji wa Polisi ya Uganda, Fred Enanga, ameeleza kuwa watu hao 20 wamekamatwa kama washukiwa washirika wa kundi la waasi la ADF lenye makao yake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Msemaji wa Polisi ya Uganda amesema miongoni mwa waliotiwa mbaroni ni pamoja na mwalimu mkuu na Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Lubiriha huko Mpondwe magharibi mwa Uganda iliyoshambuliwa usiku wa kuamkia Jumamosi.
Enanga ameongeza kuwa jumla ya watu 42 wameripotiwa kuuliwa katika hujuma hiyo wakiwemo wanafunzi 37. Amesema mhanga aliyekuwa na umri mkubwa zaidi kati ya waliouawa ni mwanamke aliyekuwa na miaka 95 huku mdogo kabisa akiwa binti wa miaka 12. Watu wengine 6 walijeruhiwa katika shambulio dhidi ya shule hiyo na hadi sasa bado wako hospitali wakipatiwa matibabu huku ripoti zenye kukinzana zikieleza kuwa, idadi ya watu waliotekwa nyara na wavamizi ni kati ya watatu na saba.
Msemaji wa polisi ya Uganda ameitaja hujuma hiyo dhidi ya watoto wasio na hatia kuwa ya kishenzi, ya kinyama na kwamba ni jinai dhidi ya binadamu.
Imebainika kuwa watu hao walikatwakatwa kwa mapanga, kupigwa risasi na kuchomwa moto hadi kufa katika mabweni yao katika mauaji ya kutisha ambayo yamelaaniwa kimataifa. Msemaji wa Polisi ya Uganda amesema, wao kama nchi wanaendelea kushirikiana bega kwa bega katika vita dhidi ya ugaidi. Amesema, waasi wa ADF hawatofanikiwa kusambaratisha umoja na mshikamano wa wananchi wa Uganda katika mapambano dhidi ya ugaidi na uchupaji mipaka haijalishi shambulizi lilikuwa la kinyama na la ukatili kwa kiasi gani.