Makumi ya magaidi wa al-Shabaab wauawa na askari wa Kenya mpakani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i99612-makumi_ya_magaidi_wa_al_shabaab_wauawa_na_askari_wa_kenya_mpakani
Makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab la Somalia wameangamizwa katika makabaliano makali baina ya wanamgambo hao na askari polisi wa Kenya mpakani mwa nchi mbili hizo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 07, 2023 03:10 UTC
  • Makumi ya magaidi wa al-Shabaab wauawa na askari wa Kenya mpakani

Makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab la Somalia wameangamizwa katika makabaliano makali baina ya wanamgambo hao na askari polisi wa Kenya mpakani mwa nchi mbili hizo.

Msemaji wa Polisi ya Kenya, Resla Onyango amesema magaidi 20 waliuawa jana Alkhamisi katika makabiliano makali ya risasi na askari wa Kikosi Maalumu cha Operesheni (SOG) katika eneo la Ogorwen kaunti ya Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya.

Amesema askari wanane wa Kenya wamejeruhiwa katika mapigano hayo ya jana Alkhamisi. Onyango amesema askari polisi hao wametwaa silaha zilizokuwa mikononi mwa magaidi hao walioangamizwa, zikiwemo bunduki kadhaa, maroketi na maguneti.

Msemaji wa Polisi ya Kenya amebainisha kuwa, mapigano yalianza baada ya magaidi wa al-Shabaab waliokuwa wamejizatiti kwa silaha nzito kuwashambulia maafisa usalama hao wa Kenya mpakani. Ameongeza kuwa makabiliano hayo yalijiri kwa saa kadhaa.

Ramani inayoonesha kaunti ya Mandera, mpaka wa Kenya na Somalia

Haya yanajiri siku chache baada ya Kenya kutangaza kuwa imeakhirisha kufungua tena mpaka wake na Somalia kufuatia wimbi la mashambulizi katika ardhi yake, yanayoripotiwa kufanywa na wanamgambo wa al-Shabaab.

Mpaka wa nchi mbili hizo ulifungwa rasmi mwezi Oktoba mwaka 2011 kufuatia mashambulizi ya wanamgambo wa al-Shabaab ambao wamekuwa wakifanya hujuma dhidi ya serikali kuu ya Mogadishu kwa zaidi ya miaka 15 sasa.