Human Rights Watch yaitaka Tunisia kuacha kuwafukuza wahamiaji na kuwaelekeza jangwani
Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch limeihimiza Tunisia kuhitimisha kile ilichokitaja kuwa "Ufukuzaji wa Umati" wa wahajiri weusi wa Kiafrika kuelekea jangwani karibu na mpaka wa Libya.
Mamia ya wahajiri kutoka eneo la chini ya jangwa la Sahara wametelekezwa katika hali mbaya huko kusini kwa Tunisia tangu baada ya kufukuzwa katika mji wa bandari wa Sfax wiki iliyopita.
Human Rights Watch imetoa taarifa hii ikikosoa vurugu zilizoshuhudiwa baada ya mazishi ya raia mmoja wa Tunisia aliyekuwa na miaka 4 aliyeuawa katika mji wa bandari wa Sfax Jumatatu iliyopita baada ya kuzuka ghasia kati ya Watunisia na wahajiri.
Sfax, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, umekuwa ukitumiwa na watu wengi kama nukta ya kuanzia safari zao kuelekea Ulaya kwa njia ya bahari. Shirika la Human Rights Watch limeeleza kuwa vikosi vya usalama vya Tunisia vimewafukuza kwa umati hadi katika eneo la mbali na la kijeshi katika mpaka wa Tunisia na Libya mamia kadhaa ya wahajiri weusi wa Kiafrika wanaotafuta hifadhi, ikiwa ni pamoja na watoto na wanawake wajawazito tangu tarehe pili mwezi huu wa Julai.

Taarifa ya HRW imeongeza kubainisha kuwa wahajiri wengi wamesema kuwa walikumbana na unyanyasaji kutoka kwa maafisa wa Tunisia wakati wa kutiwa nguvuni au kufukuzwa. Shirika hilo limeitaka serikali ya Tunisia kukomesha fukuza hiyo ya umati na kufanikisha mara moja misaada ya kibinadamu kwa wahajiri wa Kiafrika na wale wanaotafuta hifadhi ambao wamefukuzwa na kupelekwa katika eneo hatarishi.