Ulimwengu wa Spoti, Machi 3
Hujambo mpenzi mwanaspoti. Karibu tuangazie japo kwa mukhtasari baadhi ya matukio yaliyogonga vichwa vya habari katika viwanja na kumbi mbalimbali za michezo ndani ya wiki moja iliyopita...
Mieleka: Iran yatamba
Timu ya mchezo wa mieleka ya Iran imeng'ara katika Kombe la Kimataifa la Muhamet Malo mjini Tirana, Albania, na kuchota medali nne za dhahabu, moja ya fedha, na moja ya shaba katika mkondo wa pili wa msururu wa mashindano ya United World Wrestling (UWW) ya 2025. Mashindano hayo yaliyofanyika baina ya Februari 26-27, yawalishirikisha wanamieleka bora kutoka kote ulimwenguni. Iran imetamalaki mashindano hayo na kumaliza ikiwa na pointi 135, mbele ya Marekani (pointi 97) na Japan (alama 93), ikithibitisha tena kuwa ndiye simba katika pori la mieleka duniani.

Wanamieleka wa Iran walionyesha umbuji wao katika madaraja mengi ya uzani, ambapo Ali Mo’meni (kilo 57) alitwaa dhahabu baada ya ushindi wa kiufundi wa alama 5-2 dhidi ya Ayal Belolubsky wa Tajikistan katika fainali, na Rahman Amouzad (kilo 65) akionyesha udhibiti kamili katika kipindi chote cha pambano kwa kumshinda Tairbek Zhumash wa Kyrgyzstan kwa alama 5-0 na kuchota dhahabu. Medali nyingine za dhahabu ziliztwaliwa na Kamran Ghasempour wa daraja la uzani wa kilo 92 na nguli Amir-Hossein Zare’ (kg 125). Kufanya vyema nchini Albania kunaimarisha zaidi historia ya mieleka ya Iran inapojiandaa kwa mashindano yajayo ya kimataifa na Mashindano ya Dunia ya Mieleka ya 2025.
Ukweaji Barafu: Iran yaibuka ya 2
Wakweaji barafu wa Iran Mohsen Beheshti-Rad na Mohammad-Reza Safdarian wamejinyakulia medali za fedha katika Kombe la Dunia la Kupanda Barafu la Shirikisho la Kimataifa la Kukwea Barafu na Milima (UIAA), lililofanyika Edmonton nchini Canada, baina ya Februari 27 na Machi Mosi.
Wakati huo huo, wanamichezo wa Iran wametwaa medali nne katika michuano ya 33 ya Bara la Asia ya mchezo wa kuteleza kwenye theluji iliyofanyika nchini China. Katika siku ya pili na ya mwisho ya Mashindano ya Skii ya Alpine ya Asia kwa vijana wenye chini ya miaka 27, Zahra Alizadeh alishinda medali ya dhahabu kwa upande wa wanawake, huku Sarina Ahmadpour, mwakilishi mwingine wa kike kutoka Iran, akishika nafasi ya tano. Kwa upande wa wanaume, Mohammad Saveh-Shemshki alishinda medali ya shaba katika kategoria yake huku Amir-Ali Alizadeh akimaliza wa sita. Mapema Jumamosi, wanaskii wa Iran walinyakua shaba mbili.
Debi la Tehran: Persepolis yaizidi kete Esteghlal
Timu ya kandanda ya Persepolis iliiadhibu Esteghlal kwa kuizaba mabao 2-1 katika Ligi ya Wataalamu ya Ghuba ya Uajemi ya 2024/25 (PGPL) siku ya Alhamisi. Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azadi hapa Tehran, Hossein Kanaanizadegan aliipatia Persepolis bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti dakika ya 45. Alireza Kushki alisawazisha mechi hiyo kwa goli la kichwa kunako dakika ya 55. Muda mfupi baadaye, Persepolis waliwaweka wapinzani wao chini ya mashinikizo lakini bila kuona lango, lakini hatimaye Alipour alifunga bao la ushindi dakika ya 71 kwa kuvuta mkwaju kwa mguu wa kulia, ambao nusra utoboe nyavu. Watani hao wa jadi wamevaana mara 105, huku Persepolis wakiibuka kidedea mara 29, na Esteghlal mara 26.

Mechi 50 zilimalizika kwa miamba hiyo ya soka ya Iran kutoshana nguvu. Mapema Alkhamisi hiyo, vinara wa ligi, Teractor na Sepahan waliambulia sare tasa katika uwanja wa Yadegar huko Tabriz. Kadhalika, Mes iliishinda Chadormalou bao 1-0 huko Rafsanjan wakati ambapo Esteghlal ya Khuzestan ilikuwa ikipoteza kwa Malavan kwa mabao 2-1 huko Ahvaz. Watengeneza matrekta wanaongoza jedwali kwa pointi 45, pointi moja juu ya Sepahan. Persepolis wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 41. Vijana wangu wa Esteqlal naambiwa labda tuwatafute chini chini huko kuanzia nafasi ya tisa.
Israel yazidi kuchukiwa michezoni
Mashabiki wa soka wa Malaysia wamejiunga na kampeni ya 'Show Israel Red Card' yaani "Ionyeshe Israel Kadi Nyekundu" katika uwanja wa soka ili kuonyesha uungaji mkono wao kwa Palestina. Kampeni hii ya kuunga mkono Palestina dhidi ya Israel katika soka hadi sasa imetekelezwa katika nchi 30 duniani na watazamaji wa klabu 72 wameipatia Israel kadi nyekundu. Kampeni ya "Ionyeshe Israel Kadi Nyekundu" ilianza hivi karibuni wakati mashabiki wa timu ya soka ya Celtic ya Scotland walipolaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina na Lebanon katika mechi ya mkondo wa kwanza ya hatua ya mtoano ya UEFA Champions League dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani iliyochezwa Februari 12.

Mashabiki wa timu ya Celtic, maarufu kama Green Brigade waliongoza maandamano makubwa wakiwa na bango lililosema "Show Israel The Red Card," likiyataka mashirikisho ya UEFA na FIFA kuchukua hatua dhidi ya Israel katika mashindano hayo. Hivi majuzi mashabiki wa klabu ya Osasuna ya Uhispania walitoa wito wa kukomeshwa uhalifu wa utawala wa Israel huko Palestina katika mechi na mpira wa miguu iliyofanyika kati ya timu hiyo dhidi ya Real Madrid. Idadi kubwa ya mashabiki wa soka pia walifika kwenye uwanja huo wakiwa na bendera za Palestina.
Soka: Australia yatwaa Kombe la Asia
Timu ya soka ya Australia iliilemea Saudi Arabia kwenye mikwaju ya penalti na kushinda Kombe la Asia la China kwa vijana wenye chini ya miaka 20 siku ya Jumamosi. Steven Hall aliokoa mkwaju wa penalti wakati Australia ilipoilaza Saudi Arabia mabao 5-4 kwenye upigaji matuta, katika Uwanja wa Baoan Sports Center Jumamosi. Mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya 1-1 katika muda wa kawaida, mambo yakisalia vivi hivi katika muda wa ziada. Pande zote mbili zilikosa nafasi chache zilizojitokeza katika kipindi cha pili kabla ya dakika 30 za nyongeza ambazo hazikuzaa matunda, na hivyo wakaingia kwenye mikwaju ya penati.
Wakati huo huo, timu ya taifa ya Iran ilifungwa na Japan kwa mikwaju ya penalti katika robo fainali iliyopigwa Jumapili, na kuondoka kwenye michuano hiyo ya kikanda.
Na nikudokeze kuwa, mashindano ya Samia Women Super Cup yanatazamiwa kuanza kutifua mavumbi Jumanne hii ya Machi 4. Mashindano hayo yanayofadhiliwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa JMT yatazichuanisha klabu za JKT Queens, Simba Queens, Yanga Princess na Fountain Gate Princess kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Katika droo iliyofanyika karibuni, michuano hiyo itaanzia nusu fainali huku Simba Queens itavaana na JKT Tanzania katika nusu fainali ya kwanza wakati Yanga Princess itakabiliana na Fountain Gate. Kwa mujibu wa Meneja wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, mashindano hayo yataanza rasmi Machi 4. Amesema mechi ya kutafuta mshindi wa tatu itachezwa machi 6, huku fainali ikifanyika Machi 8, siku ambayo pia itakuwa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake.