Turathi zinazoibwa na utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi, Sept 9
https://parstoday.ir/sw/news/event-i131690-turathi_zinazoibwa_na_utawala_wa_kizayuni_katika_ukingo_wa_magharibi_sept_9
Karibuni wapendwa wasikilizaji wa Redio Tehran katika Makala ya Wiki ambapo leo tutazungumzia jinai ya kiutamaduni inayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kuyakalia kwa mabavu maeneo ya kale ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Utawala huo umejimilikisha turathi za utamaduni za Wapalestina kwa ajili ya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kambi zao kwa kisingizio cha kujilinda.
(last modified 2025-10-09T09:10:34+00:00 )
Oct 07, 2025 05:43 UTC
  • Turathi zinazoibwa na utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi, Sept 9

Karibuni wapendwa wasikilizaji wa Redio Tehran katika Makala ya Wiki ambapo leo tutazungumzia jinai ya kiutamaduni inayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kuyakalia kwa mabavu maeneo ya kale ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Utawala huo umejimilikisha turathi za utamaduni za Wapalestina kwa ajili ya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kambi zao kwa kisingizio cha kujilinda.

M1: Wasikilizaji wapenda kama tulivyosema, makala hii inazungumzia turathi za Wapalestina zilizoporwa na utawala wa Kizayuni katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan. Kuanzia mawe ya kale hadi kuta za zamani, misikiti na makanisa hadi katika nyumba za kihistoria za Palestina, kila moja inasimulia uporaji, kukaliwa kwa mabavu na maangamizi ya kiutamaduni.

Simulizi hii inahusu kisa cha Ukingo wa Magharibi. Eneo ambalo utawala wa Kizayuni, kupitia hatua rasmi, unaandika upya historia huku ukiiba na kupora  turathi za kitamaduni za Wapalestina. 

M2: Ripoti mpya ya Taasisi ya Utafiti ya Arij Applied Reseach katika Ukingo wa Magharibi imefichua wizi huo wa kiutamaduni unaofanywa kwa mpangilio maalumu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jeshi la utawala wa Kizayuni limetangaza maeneo 63 ya kale ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi kuwa ni "Maeneo ya Kale ya Israel"; hatua ambayo ni ukiukaji wa wazi wa sheria na mikataba ya kimataifa, na sambamba na vita na hatua za mabavu inatambuliwa kuwa ni sehemu ya mradi mkubwa wa unyang'anyi wa kitamaduni. 

M1: Kwa mujibu wa kijitabu chenye maagizo ya kijeshi kilichotiwa saini na Brigedia Jenerali Moti Almoz, mkuu wa Idara ya Masuala ya Kiraia wa Israel katika Ukingo wa Magharibi, maeneo 63 katika miji ya Nablus, Ramallah na Salfit yameainishwa kama "maeneo ya kihistoria ya Israel," hatua ambayo kwa mtazamo wa kisheria, hiana uhalali wowote isipokuwa ni unyakuzi wa ardhi.

M2: Hatua hii sio tu suala la kiutawala au kisheria, bali pia ni sehemu ya sera iliyopangwa inayolenga kufuta utambulisho wa kitamaduni wa Wapalestina na kunyakua ardhi zao kwa ajili ya upanuzi wa makazi ya walowezi wa Kizayuni, vituo vya kijeshi, na vituo vya burudani na utalii. 

M1: Ili kuweza kutambua taahira za sera hii inatosha  kutupia jicho takwimu mbalimbali. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana wa 2024, karibu walowezi wa Kizayuni 770,000 wanaishi katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na wametapakaa katika vitongoji 180 na maeneo ya kiraia 256. Vitongoji hivyo vimekata kikamilifu njia za mawasiliano za Wapalestina na hivyo kupunguza pakubwa uwezekano wa kuasisiwa nchi huru ya Palestina. 

M2: Zaidi ya hayo, utekelezaji wa miradi mikubwa kama vile mradi wa "E1", ulioidhinishwa hivi karibuni na baraza la mawaziri la Israel unatenganisha kabisa maeneo ya kaskazini na kusini mwa Ukingo wa Magharibi. Hatua hii inakwamisha njia ya kujitawala Wapalestina na kuasisi taifa lao, na wakati huo huo inaufanya urithi wa kitamaduni kuwa wenzo wa kisiasa na uvamizi na kukalia kwa mabavu ardhi za palestina.  

M1: Taasisi ya Utafiti ya Arij inasisitiza kuwa utawala wa Israel umesajili zaidi ya maeneo 2400 ya kale ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi kama "Maeneo ya Kihistoria ya Israel". Kidhahiri, hatua hii inaonekana kuwa ni katika kulinda na kuhifadhi turathi za kitamaduni, lakini kivitendo, eneo kubwa la ardhi ya Palestina limeporwa na utawala wa Kizayuni, huku  turathi za kale zikinyakuliwa kwa kisingizio cha kuendeleza utalii na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. 

M2: Katika mji wa Nablus, maeneo ya kale 59 yamevamiwa; matatu huko Ramallah na eneo moja huko Salfit. Maneeo yote haya yapo karibu na makazi au kambi za kijeshi za utawala wa Israel, kwa hivyo sera hii ni ya kimfumo kikamilifu na iliyotekelezwa kwa malengo maalumu.        MUZIKI     M1: Historia ya Palestina ni historia ya mapambano, utamaduni na utambulisho wa watu ambayo imesajiliwa kupitia athari za kale na maeneo matukufu. Hata hivyo hii leo, turathi hizo zimeporwa na kuibwa, na kila ukuta na jiwe linaloakisi utambulisho wa Palestina limeunganishwa na  historia bandia ya utawala huo na kuweka lebo feki. 

M2: Lengo la utawala wa Israel liko wazi kabisa. Ardhi ya Wapalestina inaporwa na vitongoji vya walowezi vinaendelea kujengwa katika ardhi hizo kwa kisingizio cha kulinda turathi za kale. Kwa kuendelea kutekeleza sera hii, historia ya Palestina inafutwa katika kumbukumbu, na utamulisho wao wa kitamaduni unafifia polepole. 

M1: Katika upande mwingine, sera hii ya utamaduni imeshika kasi sambamba na mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi. Tangu kuanza vita hivyo baada ya Oktoba 7,2023, Wapalestina zaidi ya 1,015 wameuawa shahidi katika Ukingo wa Magharibi na huko Quds Mashariki pekee. Wakati huo huo, Wapalestina karibu elfu saba wamejeruhiwa na zaidi ya 18,500 wametiwa nguvuni. 

M2: Tunaweza kusema kuwa sera ya utawala wa Israel ya kuiba turathi za Wapalestina ni sehemu ya mradi mkubwa zaidi wa utawala huo. Mradi huo unajumuisha kubomoa na kuharibu maeneo ya Palestina, kupora ardhi, kuanzisha vitongoji vya Wayahudi na kupunguza uwezekano wa kuunda nchi huru ya Palestina. 

M1: Kwa mujibu wa ripoti ya Arij,  baada ya kupora turathi za kale, maeneo hayo yatageuzwa kuwa kambi za kijeshi, vituo vya utalii na maeneo ya starehe kwa ajili ya utawala wa Kizayuni, na Wapalestina hawana haki ya kutumia ameneo hayo. Ni wazi kuwa, turathi za kitamaduni zimekuwa wenzo wa kuendeleza uvamizi na kuwafuta Wapalestina katika ardhi zao. 

M2: Nukta nyingine muhimu ni upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kwa miaka kadhaa sasa umekuwa mtandao tata wa vitongoji vya walowezi na maeneo ya makazi yaliyo kinyume cha sheria. Mtandao huo umekata njia za mawasiliano za Wapalestina na kubana pakubwa nuvu zao za kujistawisha kiuchumi, kijamii na kitamaduni. 

M1: Mbali na Nablus na Ramallah, maeneo kama Salfit na Bait-Laham pia yamekumbwa na mradi huo wa Israel wa kitamaduni na kijeshi. Eneo lolote linaloakisi historia ya Palestina linaweza kuvamiwa na kukakliwa kwa mabavu kwa kisingizio cha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa ajili ya shughuli za utalii. Hii ina maana kwamba, mustakabali wa kitamaduni na kihistoria wa Wapalestina uko hatarini.   MUZIKI                     MUZIKI   

M2: Hatua hizi za utawala wa Israel ni ukiukaji wa wazi wa sheria na mikataba ya kimataifa ya kulinda turathi za kitamaduni. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, hakuna nchi iliyo na haki ya kumiliki urithi wa kitamaduni wa nchi nyingine au kuutaifisha kwa kisingizio cha kujilinda. Hata hivyo sheria hizi kivitendo hazifanyi kazi mbele ya sera za utawala wa Israel.

M1: Tunachokiona leo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni ishara kuwa sera ya wizi wa turathi ni sehemu ya "mkakati wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi na maangamizi ya kiutamaduni" unaotekelezwa na utawala wa Israel.