Iran iimethibitisha kivitendo mapenzi yake ya kidugu kwa majirani na Waislamu wenzake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100982-iran_iimethibitisha_kivitendo_mapenzi_yake_ya_kidugu_kwa_majirani_na_waislamu_wenzake
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika kikao cha Jumuiya ya Urafiki baina ya Iran na Kuwait kwamba, Tehran imethibitisha kivitendo mapenzi yake ya kidugu kwa majirani na Waislamu wenzake kwenye migogoro na hali ngumu zinazotokea.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 12, 2023 12:55 UTC
  • Mohammad Toronchi Balozi wa Iran nchini Kuwait
    Mohammad Toronchi Balozi wa Iran nchini Kuwait

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika kikao cha Jumuiya ya Urafiki baina ya Iran na Kuwait kwamba, Tehran imethibitisha kivitendo mapenzi yake ya kidugu kwa majirani na Waislamu wenzake kwenye migogoro na hali ngumu zinazotokea.

Balozi Mohammad Totonchi amesema hayo na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima iko pamoja na nchi majirani zake na Waislamu duniani na imethibitisha hilo kivitendo katika nyakati ngumu na nzito zinazotokea.

Jumuiya ya Urafiki baina ya Iran na Kuwait inaundwa na shakhsia wakubwa 21 wa kiuchumi, kielmu, wa vyombo vya habari na wa masuala ya kijamii. Mwenyekiti wa jumuiya hiyo ni Sheikh Ali al Khalid al Sabah, mmoja wa watu muhimu wa familia ya kifalme ya Kuwait. 

Jumuiya hiyo ya Urafiki baina ya Iran na Kuwait imefanya sherehe maalumu kwa mnasaba wa kupelekwa balozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini humo.

Iran na Kuwait zina uhusiano mzuri na wa kidugu

 

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, katika sherehe hizo, Sheikh Ali al Khalid al Sabah amesema kwamba anamuombea mafanikio na ufanisi wa kazi balozi mpya wa Iran nchini Kuwait ili aweze kuimarisha zaidi na zaidi uhusiano wa kiudugu na wa jadi baina ya mataifa haya mawili jirani ya Waislamu.

Vilevile amesisitiza kuwa, milango iko wazi kwa wafanyabiashara na watu muhimu wa sekta mbalimbali za Iran kushiriki zaidi katika shughuli tofauti nchini Kuwait.

Kwa upande wake, Mohammad Totonchi, balozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Kuwait amesema kuwa, kushiriki kwa wingi na kwa upana zaidi watu muhimu wa kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na wa vyuo vikuu wa Iran katika kazi mbalimbali nchini Kuwait ni miongoni mwa matunda ya kuwepo Jumuiya ya Urafiki baina ya Iran na Kuwait na kusisitiza kuwa, anamuomba Mwenyezi Mungu azidi kutia nguvu udugu huo.