Iran: Taarifa ya Japan na Waarabu kuhusu visiwa vitatu haina maana
(last modified Fri, 08 Sep 2023 03:18:11 GMT )
Sep 08, 2023 03:18 UTC
  • Iran: Taarifa ya Japan na Waarabu kuhusu visiwa vitatu haina maana

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa taarifa ya pamoja iliyotolewa na Japan na nchi za Kiarabu kuhusu visiwa vitatu vya Iran vya Bu Musa, Tomb Ndogo na Tomb Kubwa na kusisitiza kuwa taarifa hiyo haina umuhimu wowote.

Huku akisisitiza kuwa visiwa hivyo vitatu daima vitasalia kuwa milki ya Iran, Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa, kutolewa ripoti kama hiyo ni kinyume na uhusiano wa kirafiki wa Iran na majirani zake. 

Amesema taarifa hiyo ya Japan na nchi za Kiarabu iliyotolewa mjini Cairo baada ya kufanyika mazungumzo baina ya pande mbili hizo haina itibari wala umuhimu wowote wa kisiasa na kisheria.

Kan'ani ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inasisitiza suala la kuendelezwa sera ya ujirani mwema na kuheshimiana, inaamini kuwa ustawi na  amani ya kanda hii ni jukumu la pamoja la nchi za eneo hilo. 

Ramani inayoonesha visiwa vitatu vya Iran katika Ghuba ya Uajemi

Ikumbukwe kuwa, nyaraka zenye itibari ya kimataifa zinathibitisha kuwa, visiwa vitatu vya Bu Musa, Tombu Ndogo na Tombu Kubwa katika Ghuba ya Uajemi ni mali ya Iran.

Kwa mfano, ramani ya jeshi la majini la Uingereza mnamo mwaka 1881 inaonyesha ramani ya Wizara ya Masuala ya Bahari ya Uingereza ya mwaka 1863 na pia ramani ya Iran iliyochorwa na Wizara ya Vita ya Uingereza mwaka1886.

Katika ramani hiyo, visiwa hivyo vimepakwa rangi ya ardhi ya Iran, na kuna mifano ya hati za kimataifa zinazoonyesha mamlaka ya Iran kwa ya visiwa hivi.