Rouhani: Ugaidi ni tishio kwa dunia nzima
Rais Hassan Rouhani wa Iran ametoa mkono wa kheri na nafaka kwa kuwadia sherehe za Idul-Fitri na kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa marais wa nchi za Kiislamu na kusema kuwa, jinamizi la ugaidi ni tishio sio tu kwa nchi jirani na marafiki wa Jamhuri ya Kiislamu katika eneo hili Mashariki ya Kati, bali kote duniani.
Rais Rouhani ameyasema hayo katika mawasiliano ya simu na marais wa Afghanistan, Turkmenistan na Azerbaijan kwa mnasaba wa kuwadia Idul-Fitr, inayoadhimishwa katika nchi nyingi duniani hii leo.
Katika mazungumzo yake na Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan, Rais Hassan Rouhani amesema ni katika sera kuu za Iran ya Kiislamu kuisaidia serikali ya Kabul na kusimama bega kwa bega na taifa la Afghanistan kwa lengo la kurejesha usalama na utulivu katika nchi hiyo, mbali na kufufua uchumi wake.
Katika mazungumzo yake na Rais Gurbanguly Berdimuhamedow wa Turkmenistan, Rais Rouhani amesema Tehran inapania kuongeza kiwango cha mabadilishano ya kibiashara na nchi hiyo hadi kufikia thamani ya dola bilioni 60 za Marekani katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
Katika mazungumzo yake ya simu na Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan, Rais wa Iran amesema taifa hili liko tayari kuimarisha uhusiano wake na Waazeri, katika nyuga za siasa, uchumi na tamaduni.