Feb 24, 2024 12:11 UTC
  • Kiongozi Mkuu:

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema, "imani juu ya Jamhuri ya Watu na Uislamu" ndio wenzo wa uthabiti na maendeleo ya Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo Jumamosi alipohutubia hadhara ya waandaaji wa Kongamano la Mashahidi 24,000 wa Mkoa wa Khuzestan (kusini-magharibi mwa Iran) na kubainisha kuwa hamasa na muujiza walioonyesha watu wa Khuzestan wakati wa Vita vya Kujihami Kutakatifu ni matokeo ya muunganiko wa juhudi za watu na imani juu ya Uislamu.
Ayatullah Khamenei ameashiria jinsi Imamu Khomeini (MA) alivyouchagua kwa umakini mkubwa msamiati wa “Jamhuri ya Kiislamu” na akasema: kilichoifanya Iran ya Kiislamu iwe na uthabiti na kusonga mbele kimaendeleo na kuvishinda vizuizi na njama chungu nzima ni kujumuishwa pamoja "imani juu ya Jamhuri ya Watu na Uislamu"; na kuendelezwa fikra hiyo ndiyo njia itakayowezesha kuyashinda matatizo katika siku za usoni pia.
 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa Idi adhimu na tukufu ya mwezi 15 Sha'bani na akaashiria utambuzi makini aliokuwa nao Imamu Khomeini (MA) juu ya watu, pamoja na mtazamo wake mpana na wa kimaendeleo kuhusu Uislamu na akasema, Imam Khomeini (MA) alikuwa na imani na wananchi tangu mwanzo kabisa wa harakati ya Kiislamu hadi ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na baada ya hapo pia; na alikuwa akiuchukulia Uislamu kuwa ni njia ya fikra yenye ufanisi kwa ajili ya siasa na uendeshaji wa jamii, na kwa kuzingatia hayo akaweza kuandaa mazingira kwa ajili ya maendeleo ya Iran na kuendelezwa harakati zingine kubwa.
Hadhirina wakisikiliza hotuba ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, tatizo kubwa zaidi la maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ni kutokuwa na uelewa wa kuwatambua watu wa Iran na kutoufahamu Uislamu pia na akabainisha kwamba, kwa kutegemea makadirio na mipango yao, maadui wa taifa la Iran walikuwa na uhakika kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaushuhudia mwaka wake wa 40, lakini tamaa yao imeambulia patupu kwa sababu maendeleo ya Iran hayatasita bali yataendelea kwa rehma za Mwenyezi Mungu na kwa kutegemea hima, juhudi na irada ya wananchi na imani yao juu ya dini.

 
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, hali ya leo ya Wapalestina ni kielelezo kingine cha muujiza unaotokana na kuwategemea wananchi na imani ya dini na akafafanua kwamba: kusimama imara vikosi vya Muqawama na kukatishwa tamaa adui ya kuweza kuviangamiza vikosi hivyo, na vilevile subira iliyoonyeshwa na watu wa Ghazza mbele ya mashambulio ya mabomu na misiba na masaibu yanayowapata, ni ishara ya imani kubwa na thabiti ya dini waliyonayo watu hao.
 
Ayatullah Khamenei ameashiria pia kudhihirika uwongo wa madai ya Ustaarabu wa Magharibi kuhusu haki za binadamu na uzandiki wa kimaonyesho na unafiki wa Wamagharibi katika kadhia ya Ghazza na akasema: Wamagharibi wanaozusha zogo na makelele anaponyongwa mhalifu mmoja tu, wamefumba macho yao mbele ya mauaji ya watu 30,000 wasio na hatia katika Ukanda wa Ghazza; na kwa ujeuri mkubwa Marekani imepinga tena kwa mara nyingine azimio la kukomesha mashambulio dhidi ya Ghazza.
Hadhirina wakisikiliza hotuba ya Ayatullah Khamenei

Amesisitiza kwa kusema: "hii ndio sura halisi ya utamaduni na ustaarabu wa demokrasia ya kiliberali ya Magharibi, ambayo kwa nje yake unawaona wanasiasa wanaotabasamu wakiwa wamevalia suti maridadi, lakini kwa ndani yake, watu hao ni mbwa vichaa na mbwa mwitu wenye uchu wa damu".

 
Kwa kumalizia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: "tuna uhakika kwamba ustaarabu huu wa Kimagharibi na shehena hii mbovu haitafika ilikokusudiwa kupelekwa; na utamaduni wa kweli na mantiki sahihi ya Uislamu itayashinda yote haya".../

Tags