Mar 23, 2024 07:45 UTC
  • Msemaji wa AEOI: Iran inahitaji vituo 20 vya nyuklia

Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema Jamhuri ya Kiislamu inapasa kuwa na vituo kati ya 15 na 20 vya nyuklia ili kujidhaminia mahitaji yake ya nishati.

Shirika la habari la Tasnim limemnukuu Behrouz Kamalvandi akiyasema hayo kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa Kiirani wa 1403 Hijria Shamsia na kuongeza kuwa, shughuli zote za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu zinafanyika kulingana na sheria.

Amebainisha kuwa: Kuna vituo 500 vya nishati ya atomiki kote dunia hivi sasa. Kwa msingi wa maamuzi ya mkutano wa COP28, idadi ya vituo hivi inafaa kuongezeka hadi 1,500 kufikia mwaka 2050. Hisa ya Iran kwenye idadi hiyo ni baina ya 10 na 12.

Hata hivyo Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesisitiza kuwa, Iran haina nia ya kuunda silaha za nyuklia na inachofuatilia daima ni kuzalisha nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani na ya kiraia.

Amesema mafanikio ya teknolojia ya nyuklia ya Iran yanalenga kuleta amani na kutoa huduma kwa wanadamu. Kamalvandi ameeleza bayana kuwa, shughuli zote zinafanywa kwa kuzingatia viwango na kanuni za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Kituo cha kuzalisha nishati ya nyuklia cha Iran

Msemaji wa taasisi ya nyuklia ya AEIO ya Iran ameashiria vikwazo vya maadui dhidi ya Iran na kusisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu inapinga kila aina ya ubeberu na ukiritimba wa sayansi na teknolojia.

Amesema Iran itayashirikisha mashirika ya kigeni katika ujenzi wa vituo hivyo vipya vya nyuklia, na kwamba tayari inaendelea kuzungumza na China na Russia ili kufanikisha mpango huo.

Tags