Apr 16, 2024 10:49 UTC
  • Ebrahim Raisi: Hatua yoyote dhidi ya Iran itapata majibu makali

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hatua yoyote hata ndogo kiasi gani itakayochukuliwa dhidi ya manufaa ya Iran, bila ya shaka yoyote itapata majibu makali na ya kuumiza kwa wote watakaohusika na hatua hiyo.

Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo katika mazungumzo ya simu na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani na huku akiashiria matukio ya hivi karibuni kwenye eneo hili amesema kuwa tukio muhimu zaidi hivi sasa katika ukanda wa Asia Magharibi na hata dunia nzima, ni kuendelea mauaji ya kimbari na ya kikatili ya Israel dhidi ya Wapalestina na udharura wa kufanyika juhudi zaidi ya kuhakikisha utawala wa Kizayuni unakomesha jinai zake.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, mauaji ya watoto, uangamizaji wa kizazi na jinai za kutisha za Wazayuni zinafanyika kwa uungaji mkono kamili wa Marekani na baadhi ya madola ya Magharibi lakini wananchi madhlumu lakini walio imara wa Ghaza bado ndio washindi kutokana na muqawama wao wa kupigiwa mfano.

Rais Raisi pia amesema, baada ya utawala wa Kizayuni kuushambulia ubalozi wa Iran mjini Damascus, Umoja wa Mataifa umeshindwa kutimiza hata sehemu ndogo kabisa ya jukumu lake kama ulivyoshindwa kutekeleza majukumu wake kuhusu kukomesha mauaji ya umati  huko Ghaza, hivyo Jamhuri ya Kiislamu haikuwa na njia nyingine isipokuwa kutumia haki yake ya kujilinda na kutoa majibu makali kwa jinai ya utawala wa Kizayuni.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani amesema kuwa wakati huu ambapo dunia nzima iko pamoja na wananchi wa Palestina, utawala wa Kizayuni unafanya njama za kuhatarisha usalama wa eneo hili ili kuwashughulisha walimwengu na masuala mengine na kuwasahaulisha kadhia ya Palestina.