Apr 17, 2024 10:49 UTC
  • Iran iliwasiliana na nchi za eneo katika kutekeleza Operesheni ya Ahadi ya Kweli dhidi ya Israel

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema: Iran ilikuwa ikiwasiliana na nchi za eneo katika mchakato wa kutoa jibu kwa utawala wa Kizayuni na utekelezaji wa Operesheni ya Ahadi ya Kweli.

Jumatatu ya Aprili Mosi, utawala wa Kizayuni ulifanya shambulio la kigaidi dhidi ya sehemu ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, Syria lililopelekea kuuawa shahidi washauri saba waandamizi wa kijeshi wa Iran.
Kufuatia jinai hiyo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran alitangaza kuwa hatua ya Tel Aviv ni sawa na kushambulia ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasisitiza kuwa utawala wa Kizayuni "utatiwa adabu".
 
Mnamo usiku wa kuamkia Jumapili ya tarehe 14 Aprili, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilichukua hatua ya kuutia adabu utawala huo mchokozi katika Operesheni ya Ahadi ya Kweli iliyohusisha ndege zisizo na rubani na makombora yaliyoshambulia vituo vya kijeshi vya utawala huo haramu.

Kuhusiana na hilo, Ali Bagheri, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshusika na masuala ya kisiasa amesema katika mahojiano maalumu ya habari na Chaneli ya Pili ya Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu kwamba, "suala kuu lililosisitizwa kwa muda wote huu ni kwamba, Iran haitaki kuzusha mivutano; na kwa muda wote wa miezi saba iliyopita tumetumia uwezo wetu wote kuanzia kitaifa, kikanda na kimataifa ili mvutano uliopo usisambae katika eneo".

 
Bagheri ameongeza kuwa, kutokana na sera yake ya kuwa na ujirani mwema, kwa muda wote huu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanya mawasiliano mengi na ya kudumu na nchi jirani; na hii ni rasilimali yenye thamani kubwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kukabiliana na adui wa eneo ambaye daima analenga kuvuruga na kuondoa uthabiti katika eneo hili na ameweza kila mara kufuatilia malengo yake haramu kwa ubabe na utumiaji mabavu.
 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshusika na masuala ya kisiasa amebainisha kuwa, nchi kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nguvu na uwezo na ina irada pia ya kutowaruhusu wale wanaovuruga usalama wa eneo wasivuruge usalama wa eneo hili; na Iran haitamruhusu mtu yeyote afanye uafriti, kosa au uwendawazimu katika eneo; na gharama ya kuvuruga utulivu lazima ilipwe na mvurugaji.../

 

Tags