Apr 27, 2024 13:18 UTC
  • Wanafunzi wa Chuo Kikuu Tehran waandamana kuunga mkono maandamano ya wenzao wa Marekani

Wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Tehran wamefanya maandamano leo Jumamosi kuunga mkono maandamano yanayoongezeka kwenye kampasi za Marekani ambapo wanafunzi wamepiga kambi wakitaka kukomeshwa vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza huko Palestina.

Wakipiga nara za "kifo kwa Marekani, "kifo kwa Israel" na "kifo kwa Uingereza", waandamanaji hao wamelaani mashambulizi makali ya polisi wa Marekani dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu.

Shirika la Habari la Iran (IRNA) limeripoti kuwa, maandamano hayo yalikuwa onyesho la "kuungaji mkono mwamko wa jumuiya ya wasomi wa Marekani na Ulaya katika kukemea ukatili na mauaji ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina yanayofanywa na utawala bandia wa Israel na uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo unaoua watoto."

Maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Marekani kupinga vita vya Israel dhidi ya Gaza yaliongezeka na kupanuka zaidi wiki iliyopita baada ya polisi kuwatia nguvuni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Columbia.

Polisi wakikabiliana na waandamanaji Marekani

Kambi za kuonyesha mshikamano na watu wa Gaza zimeanzishwa katika vyuo vikuu, ikiwa ni pamoja na Yale, na Chuo Kikuu cha New York. Polisi wameitwa katika vyuo kadhaa kuwakamata mamia ya wanafunzi wanaoandamana.

Maandamano hayo yamekuwa ya amani, lakini yamekabiliwa na hatua kali za polisi na serikali ya Marekani inayoendelea kufadhili mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina.

Katika vyuo vikuu ambako maandamano yanafanyika, wanafunzi wametoa wito wa kusitishwa mapigano kwa njia ya kudumu huko Gaza, kukomeshwa misaada ya kijeshi wa Marekani kwa Israel, vyuo vikuu vya Marekani kuondolewa chini ya udhibiti wa wauzaji silaha na makampuni mengine yanayonufaika kutokana na vita, na kusamehewa wanafunzi na wafanyakazi walioadhibiwa au kufukuzwa kwa sababu ya kuandamana kuwatetea watu wa Gaza.